Dec 04, 2020 04:32 UTC
  • Utawala wa Kizayuni  na mkakati wa kubadili muundo wa kijamii katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu

Ikiwa ni katika jitihada za kubadili muundo wa kijamii huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu; viongozi wa utawala wa Kizayuni wametangaza kuwa mamia ya wahajiri wa Kiyahudi wenye asili ya Ethiopia jana Alhamisi wamewasili Tel Aviv.

Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel Benjamin Netanyahu, Waziri wa Vita Ben Gantz na Gaby Ashkenaz Waziri wa Mambo ya Nje wa utawala huo jana waliwalaki wahajiri hao wa Kiethioia katika uwanja wa ndege wa Ben Gurion. Tovuti ya habari ya al Rai al Yaum imeashiria kuwasili wanawake na watoto wengi wahajiri wa Kiyahudi kutoka Ethiopia na kuandika kuwa hatua hiyo imejiri katika kalibu ya mkakati wa kuwapatia makazi katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu Wayahudi elfu mbili wa Kiethiopia. 

Netanyahu akiwapokea wahajiri wa Kiyahudi kutoka Ethiopia 

Sambamba na kuwasili huko Tel Aviv wahajiri hao kutoka Ethiopia; Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni ameandika katika ukurasa wake wa twitter kwamba, wahajiri 100 wengine wa Kiyahudi pia leo Ijumaa watawasili Tel Aviv; na  hadi kufikia  mwanzoni  mwa mwaka ujao wa 2021 wahajiri hao watakuwa wamefikia elfu mbili.  

Baraza la mawaziri la utawala wa Kizayuni mwezi Oktoba mwaka huu lilipasisha mpango wa kuwapatia makazi Wayahudi wa Kiethiopia wapatao elfu mbili.  Televisheni ya Kizayuni pia imeripoti kuwa, hadi sasa kuna jumla la Wayahudi wa Kiethiopia elfu 95 ambao katika miaka ya karibuni wamehajiri huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu.

Tags