Dec 07, 2020 01:17 UTC
  • Emir wa Kuwait akubali hatua ya serikali kujiuzulu

Emir wa Kuwait Sheikh Nawaf Al-Ahmad Al-Jaber Al-Sabah ameafiki hatua ya kujiuzulu serikali ya nchi hiyo. Kujiuzulu serikali nchini Kuwait ni jambo la kawaida ambalo hufanyika baada ya uchaguzi. Siku ya Jumamosi uchaguzi wa bunge ulifanyika nchini Kuwait.

Kwa mujibu wa taarifa, Waziri Mkuu wa Kuwait Sabah Al Khalid Al Sabah  aliwasilisha barua ya kujiuzulu serikali yake siku ya Jumapili.

Aidha amelitaka baraza  la mawaziri lililopo kuendelea kushikilia nyadhifa kwa muda hadi serikali mpya itakapoundwa. 

Waziri Mkuu Al Khalid Al Sabah amesema uchaguzi wa bunge jipya la kitaifa ulifanyika kwa njia huru na ya haki pamoja na kuwekwa mipaka mingi kutokana na janga la COVID-19.

Wananchi wa Kuwati walishiriki katika uchaguzi wa bunge Jumamosi huku nchi hiyo ya Ghuba ya Uajemi ikikabiliwa na mgogoro mbaya zaidi wa kiuchumi kuwahi kushuhudiwa kwa miongo kadhaa. Serikali imekuwa ikililaumu bunge kuwa linapinga sera za marekebisho. 

Bunge la Kuwait

Kulikuwa na wagombea 326 waliokuwa wakiwania viti 50 katika bunge la nchi hiyo.

Emir wa sasa wa Kuwait, Sheikh Nawaf, 83, alishika madaraka baada ya kufa ndugu yake aliyekuwa Amir, Sheikh Swabah, mwezi Septemba akiwa na umri wa miaka 91.

 

Tags