Dec 15, 2020 11:34 UTC
  • Kuwait: Jukumu la usalama wa Ghuba ya Uajemi ni la nchi zote za eneo hilo

Waziri Mkuu wa Kuwait amesema kuwa, suala la kulinda usalama wa Ghuba ya Uajemi ni jukumu la nchi zote za eneo hilo na hakuna nchi yoyote inayoweza kujivua na jukumu hilo.

Televisheni ya al Jazeera ya Qatar imemnukuu Sabah al Khalid al Sabah akisema hayo wakati akifungua bunge la 16 la nchi hiyo na kuongeza kuwa, nchi wanachama wa Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajeni zitashiriki katika kudhamini usalama wa eneo hilo.

Waziri Mkuu wa Kuwait amegusia ugomvi mkubwa uliopo baina ya wanachama wa baraza hilo hususan baina ya Saudi Arabia na Qatar na kusema kuwa, nchi yake haitosita kufanya juhudi zozote zinazotakiwa za kuweza kuondoa ugomvi na mzozo huo.

Eneo la Ghuba ya Uajemi

 

Tarehe 5 Juni 2017, Saudia, Imarati, Bahrain na Misri zilikata uhusiano wao wote na Qatar kwa madai kuwa Doha inaunga mkono ugaidi. Tangu mwaka huo hadi hivi sasa nchi hizo nne za Kiarabu zimeifungia Qatar njia zote za ardhini, baharini na angani. 

Nchi hizo zimeweka masharti 13 mazito ya kuweza kurudisha uhusiano wao wa kawaida na Qatar. Baadhi ya masharti hayo mazito ambayo ni muhali kuweza kukubaliwa na nchi hiyo, ni kuitaka Doha ikate uhusiano wake na Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS, ivunje uhusiano wake wa Uturuki, ifunge kambi za kijeshi za Uturuki nchini humo, iivunje televisheni ya al Jazeera na masharti mengine mengi magumu.

Qatar imekataa katakata kutekeleza masharti hayo ikisisitiza kuwa yanalenga moja kwa moja kwenye haki ya kujitawala nchi hiyo.

Tags