Dec 18, 2020 06:01 UTC
  • Mapatano ya Riyadh yagonga mwamba;  vita vya mafuta  kati ya Saudia na Imarati vimeanza huko Yemen

Gazeti moja linalochapishwa kwa lugha ya Kiarabu limeripoti juu ya kuendelea kugonga mwamba mapatano yaliyofikiwa na Riyadh huko Yemen na kuibuka hitilafu kali kati ya nchi hiyo na Imarati kuhusu umiliki wa mafuta nchini humo.

Gazeti la Al Akhbar jana liliripoti kuwa, ni sehemu ndogo tu ya hatua za kijeshi ndani ya mapatano hayo ya Riyadh ndiyo imekwishatekelezwa hadi sasa; na kwamba kuanzia sasa kuna uwezekano wa kuwa mbaya hali ya mambo kati ya pande mbili hizo kutokana na hitilafu zilizo nyuma ya pazia kati ya Riyadh na Abu Dhabi huko kusini mwa Yemen. 

Gazeti la al Akhbar limeandiaka kuwa, mkoa tajiri kwa mafuta wa Shabwah ni moja ya mambo yaliyobua hitilafu kati ya Abu Dhabi na Riyadh kuhusu nani anapasa kumiliki utajiri wa eneo hilo; na katika upande mwingine mivutano kati ya mamluki wenye mfungamano na Imarati na Saudia katika mkoa wa Abyan kusini mwa Yemen ingali inaendelea.  

Gazeti hilo la Kiarabu limeashiria namna mapigano yanayoendelea kuhusu umiliki wa mkoa wa Shabwah na katika mikoa mingine yenye mafuta huko Yemen yalivyochukua mkondo wa kimataifa pia na kusisitiza kuwa, katika vita dhidi ya Yemen nchi za Magharibi zinayatazama tu maslahi yake maalumu khususan kuziuzia silaha nchi za Kiarabu za pambizoni mwa Ghuba ya Uajemi kwa lengo la kupora mafuta ya Yemen. 

Vita vya kuwania mafuta nchini Yemen kati ya Saudia na Imarati 

Saudi Arabia inafanya juhudi za kutekeleza sehemu ya kijeshi ya mapatano hayo ya Riyadh lakini Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) kwa upande wake hautaki kutekeleza mapatano hayo kabla ya kujulikana hatima ya mkoa wa Shabwah. 

Mapatano ya Riyadh ni mapatano yaliyofikiwa na Saudi Arabia na Imarati kwa lengo la kugawana madaraka na kuhitimisha mapigano ya mamluki wa pande mbili hizo huko kusini mwa Yemen; mapatano ambayo yalisainiwa tarehe 5 mwezi Oktoba mwaka huu kati ya waitifaki wao huko Riyadh. 

 

Tags