Dec 22, 2020 13:02 UTC
  • Dubai imegeuzwa kitovu cha maovu na ufuska kwa ajili ya watalii kutoka Israel

Duru za habari za lugha ya Kiebrania zimeripoti kuwa, Dubai imegeuzwa mji wa kufanyia maovu na ufuska na kuwafanya wazayuni wawe na hamu kubwa ya kuutembelea.

Kwa mujibu wa toleo la leo la gazeti la Al-Qudsul- Araby, kanali ya 13 ya televisheni ya utawala wa Kizayuni imeeleza katika ripoti kwamba, mapatano ya kuanzisha uhusiano wa kawaida kati ya Imarati na utawala wa Israel, yameigeuza Dubai kuwa kituo chenye mvuto kwa wazayuni, kiasi kwamba hoteli za mji huo zimegeuzwa kuwa kitovu cha matumizi ya pombe na madawa ya kulevya.

Kanali hiyo imeongeza kuwa, wanaharakati wa kijamii wametoa miito mara kadhaa kwa baraza la mawaziri la utawala wa Kizayuni kulitaka lipige marufuku safari za kuelekea Imarati kwa kuhofia kuongezeka maambukizo ya virusi vya corona, lakini Tel Aviv haioneshi kuwa na dhamira ya kuchukua hatua kwa kuchelea kuzuka mgororo wa kidiplomasia kati yake ya Abu Dhabi.

Wakati huohuo gazeti la Yediot Ahronot limeeleza katika utafiti liliofanya kwamba, tangu uliposainiwa mkataba wa mapatano, utalii wa ufuska mjini Dubai umeshamiri kwa vijana kutoka Israel.

Mbali na hayo, kanali ya 12 ya televisheni ya utawala wa Kizayuni iliripoti kitambo kifupi nyuma kuwa, tangu yalipoanza kutekelezwa mapatano yaliyofikiwa kati ya Imarati na utawala huo, wahalifu kadhaa Waisraeli ambao wanasakwa kwa kuhusika na kesi za mauaji na biashara haramu ya mihadarati wamekimbilia Dubai.

Imarati imekuwa nchi ya kwanza ya Kiarabu ya Ghuba ya Uajemi, ambayo mnamo Agosti 13 mwaka huu ilitangaza rasmi kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel kwa upatanishi wa serikali ya Rais Donald Trump wa Marekani.../

Tags