Jan 03, 2021 02:54 UTC
  • Wairaq kufanya maandamano mamilioni leo kukumbuka siku waliyouawa shahidi makamanda wa muqawama

Mbunge wa mrengo wa As-Sadiqun katika bunge la Iraq amesema, lengo la maandamano makubwa yatakayofanywa leo na wananchi wa Iraq kwa mnasaba wa kukumbuka siku walipouliwa shahidi makamanda wa muqawama ni kutangazwa upinzani dhidi ya uwepo kijeshi wa Marekani katika ardhi ya nchi hiyo.

Muhammad al-Baldawi amekiambia kituo cha habari cha al-Ma'lumah kwamba, leo Januari 3, inayosadifiana na siku aliyouawa shahidi Luteni Jenerali Qassem Suleimani, Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu na Abu Mahdi al-Muhandis, Naibu wa Mkuu wa jeshi la kujitolea la wananchi la Al-Hashdu-Sha'abi, maandamano makubwa yatafanyika katika mji mkuu Baghdad na mikoa mingine ya Iraq.

Al-Baldawi amebainisha kuwa, ujumbe wa maandamano ya wananchi wa Iraq katika kumbukumbu ya mwaka wa kwanza tangu walipouawa shahidi makamanda wa muqwama ambayo ni kutaka mamlaka ya kujitawala ya nchi hiyo yalindwe na kulipizwa kisasi cha damu ya mashahidi hao, unadhihirisha hisia halisi za utaifa za wananchi hao katika kupinga kuwepo wanajeshi wa Marekani katika ardhi ya Iraq.

Shahidi Qassem Soleimani (kulia) na Shahidi Abdu Mahdi al-Muhandis

Maandamano hayo ya leo yatafanyika katika uwanja wa mzunguko wa At-Tahrir mjini Baghdad kwa kaulimbiu ya "Kufa Shahidi na Kujitawala" ili kutilia mkazo ulazima wa kuwatimua askari vamizi wa Marekani na kurejesha mamlaka ya kujitawala ya Iraq.

Kabla ya hapo, Abu Dhiyaa As-Saghir, mkuu wa ofisi za Al-Hashdu-Sha'abi katika mikoa yote ya Iraq alitangaza kuwa, ratiba muhimu zaidi iliyoandaliwa kwa ajili ya maadhimisho ya siku waliyouawa shahidi makamanda wa ushindi dhidi ya ugaidi ni maandamano ya mamilioni ya wananchi mjini Baghdad na katika miji mingine mbalimbali ya Iraq, ambapo sisitizo kubwa katika maandamano hayo litakuwa ni kuondolewa mara moja askari wa jeshi la Marekani nchini humo.  

Alfajiri ya kuamkia siku kama ya leo mnamo Januari 3,2020 Luteni Jenerali Qassem Soleimani, Mkuu wa Kikosi cha Quds, cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu IRGC, Abu Mahdi al Muhandis, Naibu wa Mkuu wa Harakati ya al Hashd al Shaabi na wanamapambano wenzao wanane, waliuliwa kigaidi na kidhulma na wanajeshi magaidi wa Marekani, katika shambulio la anga lililofanywa na magaidi hao karibu na uwanja wa ndege wa Baghdad nchini Iraq.../

Tags