Jan 13, 2021 14:31 UTC
  • Shirika la Emirates lamfuta kazi rubani Mtunisia aliyekataa kurusha ndege kuelekea Israel

Shirika la Ndege la Umoja wa Falme za Kiarabu, Emirates Airline, limemfuta kazi rubani wake mmoja raia wa Tunisia ambaye alikataa amri ya kurusha ndege kuelekea Israel.

Rubani Mtunisia Monem Sahib al-Taba ameandika katika ukurasa wake wa Facebook kuwa, Shirika la Ndege la Emirates limemsimamisha kazi kutokana na uamuzi wake wa kukataa amri ya kuwa miongoni mwa marubani waliotakiwa warushe ndege ya shirika hilo kwenda Tel Aviv.

Katika ujumbe wake amesema kuwa: "Ni Mwenyezi Mungu tu anayeweza kunilinda...mimi sijutii uamuzi wangu."

Wanaharakati katika nchi za Kiarabu wamelaani vikali Shirika la Ndege la Emirates kwa kumsimisha kazi rubani huyo. Aidha wamemsifu al-Taba kwa ajili ya msimamo wake wa kishujaa wa kukataa kuutambua utawala haramu wa Israel hata baada ya Umoja wa Falme za Kiarabu kuanzisha uhusiano na utawala huo wa Kizayuni.

Wakuu wa UAE, Bahrain, utawala haramu wa Israel na rais wa Marekani Trump wakati wa kutiwa saini mapatano ya kuanzishwa uhusiano wa nchi hizo za Kiarabu na Israel

Punde baada ya kutiwa saini mkataba huo wa kuanzisha uhusiano Septemba mwaka jana, mashirika ya ndege ya Israel yalianza safari za moja kwa moja baina ya Tel Aviv na Dubai. Aidha mashirika ya ndege ya Umoja wa Falme za Kiarabu nayo pia yameanzisha safari za kuelekea Tel Aviv hatua ambayo inapingwa vikali na wananchi wa kawaida lakini wengi hawawezi kuzungumza kwa kuhofia watawala wao ambao ni makatili.

Mwaka wa 2020, nchi nne za Kiarabu ambazo ni Umoja wa Falme za Kiarabu, Bahrain, Sudan na Morocco zilitangaza kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel na hivyo kujiunga na Misri na Jordan ambazo zinautambua utawala huo ghasibu. Hatua hiyo imetajwa kuwa ni usaliti na inaendelea kulaaniwa na kupingwa na wananchi waliowengi wa nchi hizo ambao wanaitazama kuwa ni kusaliti harakati za kupigania ukombozi wa Palestina.

 

Tags