Jan 15, 2021 14:04 UTC
  • Israel yatishia kuishambulia Iran iwapo Biden atairejesha US katika JCPOA

Mpambe wa karibu wa Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni ametishia kuwa huenda Israel ikaishambulia kijeshi Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iwapo serikali ijayo ya Marekani itarejea katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA.

Tzachi Hanegbi, Waziri Ushirikiano wa Kieneo wa utawala haramu wa Israel ambaye ni mwanasiasa wa karibu na Netanyahu amemtaka Rais mteule wa Marekani, Joe Biden eti asijikombe kwa Iran kwa kuirejesha Washington katika mapatano hayo ya kimataifa, na kwamba ikilazimu Tel Aviv itashambulia miradi ya nyuklia ya Iran.

Katika mahojiano na shirika la la habari la Kan la Israel, mwanasiasa huyo mwenye misimamo mikali amebainisha kuwa: Iwapo serikali ya Marekani itarejea katika mapatano ya nyuklia, na hiyo kwa sasa inaonekana kuwa ndiyo sera rasmi ya serikali ijayo ya Washington, basi matokeo yake ni kuwa Israel itasalia pekee dhidi ya Iran.

Amedai kuwa, iwapo Washington itarejea katika JCPOA, basi itakuwa imeipa taa ya kijani Iran iendelee na eti mradi wake wa kuzalisha silaha za nyuklia. Mpambe huyo wa karibu na Netanyahu ameongeza kuwa, "Israel haitaruhusu hilo lifanyike, tayari tumeshafanya kile kilichohitajika kufanywa mara mbili huko nyuma, mwaka 1981 tulizima mradi wa nyuklia wa Iraq na mwaka 2007 dhidi ya Syria.

Sehemu ya silaha za nyuklia za utawala haramu wa Israel

Hii ni katika hali ambayo, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mara zote imekuwa ikisisitiza kuwa, miradi yake ya nyuklia ni ya kiraia na yenye malengo ya amani, jambo ambalo limethibitishwa mara chungu nzima katika ripoti za Wakala wa Kimataifa wa Niashati ya Atomiki (IAEA). 

Israel inatoa tuhuma na bwajabwaja hizo dhidi ya miradi ya nyuklia yenye malengo ya kiraia ya Iran katika hali ambayo, utawala huo pandikizi unaoua Wapalestina kila leo unamiliki mamia ya vichwa vya silaha za atomiki.

Tags