Jan 16, 2021 13:41 UTC
  • Israel inayahofu makombora yenye shabaha kali ya Hizbullah ya Lebanon

Mchambuzi wa masuala ya kijeshi wa utawala haramu wa Kizayuni wa Israel amesema, utawala huo umeingiwa na hofu na kiwewe kwa sababu ya makombora yenye shabaha kali ya harakati ya muqawama wa Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon.

Alon Ben David, mchambuzi na mhakiki wa masuala ya kijeshi ya utawala wa Kizayuni ameeleza katika makala yake iliyochapishwa katika toleo la jana la gazeti la Kizayuni la Maariv kwamba, makombora ya Hizbullah ya Lebanon yanao uwezo wa kusambaratisha na kulemaza mitambo ya kistratejia ya kiulinzi ya utawala huo haramu.

Ben David amekiri na kusisitiza kuwa, jitihada zote zilizofanywa na utawala haramu wa Israel kwa madhumuni ya kuizuia Hizbullah isiyapate makombora hayo iliyonayo hivi sasa zimegonga mwamba.

Mchambuzi huyo wa masuala ya kijeshi ya utawala wa Kizayuni amebainisha kwamba, jeshi la Israel linaitakidi kuwa, makombora yenye shabaha kali yaliyoko ndani ya Lebanon dhidi ya Israel ni tishio la kistratejia; na kwa kutumia makombora hayo, Hizbullah ina uwezo wa kukilenga kituo cha HaKirya kilichoko Tel Aviv, katika eneo ilipo wizara ya Intelijensia pamoja na makao makuu ya jeshi hilo.

Sayyid Hassan Nasrullah

Itakumbukwa kuwa mwishoni mwa mwaka uliomalizika wa 2020, Sayyid Hassan Nasrullah, Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon alisistiza kuwa, idadi ya makombora ya Muqawama yenye shabaha kali imeongezeka maradufu kulinganisha na mwaka wa kabla yake na kwamba Muqawama unao uwezo wa kuilenga kwa shabaha makini sehemu yoyote ile ya ardhi ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu iliyopewa jina la Israel.

Kabla ya hapo, aliyekuwa waziri wa vita wa utawala wa Kizayuni Avigdor Lieberman alikiri kuwa, Hizbullah ni jeshi imara na lenye nguvu katika eneo la Asia Magharibi.

Aidha mwanzoni mwa mwezi huu wa Januari, kituo cha tafiti za usalama wa ndani cha utawala haramu wa Kizayuni wa Israel kilitangaza kuwa tishio kubwa zaidi kwa utawala huo katika mwaka huu wa 2021 ni makombora yenye shabaha kali ya Lebanon, Syria, Yemen na Iran.../

Tags