Jan 17, 2021 07:55 UTC
  • Wayemen waandamana kuilaani Marekani kwa kuiweka Ansarullah katika orodha nyeusi

Wananchi wa Yemen wamefanya maandamano katika mkoa wa Sa'ada, kaskazini magharibi mwa nchi kulaani hatua ya Marekani ya kuliweka jina la Ansarullah katika orodha yake ya makundi ya kigaidi na kuitaka ifutilea mbali uamuzi wake huo.

Waandamanaji hao wamesema hatua hiyo ya Marekani dhidi ya kundi hilo la kujitolea la wananchi wa Yemen imetokana na mashinikizo ya Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu, ambazo zinaongoza muungano vamizi wa kijeshi katika vita dhidi ya Wayemen.

Baadhi ya mabango yaliyokuwa yamebebwa na waandamanaji hao yalikuwa na jumbe zinazoitaja Marekani kuwa 'Mama wa ugaidi' na chimbuko la migogoro na jinai zote zinazoshuhudiwa katika kona mbali mbali za dunia.

Kadhalika wananchi wa Yemen wametumia maandamano hayo kulaani hatua ya muungano katili wa kijeshi unaoongozwa na Saudia, ya kuendelea kumwaga damu za Wayemen mbali na kuharibu miundombinu ya nchi hiyo maskini ya Kiarabu.

Wanamapambano wa Ansarullah ya Yemen

Hatua hiyo ya Marekani ya kuliweka jina la Ansarullah katika orodha yake nyeusi ya eti makundi ya kigaidi imelaaniwa vikali ndani na nje ya Marekani, wakiwemo hata waitifaki wa Washington.

Marekani imekataa ombi lililotolewa na Umoja wa Mataifa la kufutilia mbali uamuzi wake huo wa kuiweka harakati ya Ansarullah ya Yemen katika orodha ya makundi yanayotuhumiwa na Washington kuwa ni ya kigaidi.

Tags