Jan 18, 2021 04:49 UTC
  • Mabadiliko katika stratijia ya kijeshi ya Marekani Asia Magharibi

Marekani imetoa huduma kubwa kwa utawala haramu wa Israel katika kipindi cha utawala wa Rais Donald Trump wa Marekani.

Hivi sasa pia ikiwa ni katika siku zake za mwisho mwisho za Trump kuhudumu katika ikulu ya White House, utawala wake umechukua hatua nyingine ya kudhamini maslahi ya utawala huo ghasibu.

Ijumaa tarehe 15 Januari, Wizara ya Ulinzi ya Marekani Pentagon, ilitoa taarifa ikisema kuwa imeitoa Israel katika kamandi ya usimamizi wake wa kijeshi wa eneo la Ulaya EUCOM na kuiweka katika kamandi kuu ya nchi hiyo CENTCOM. Taarifa hiyo imedai kwamba kupungua mivutano kati ya utawala ghasibu wa Israel na majirani zake wa Kiarabu kufuatia mapatano ya hiana ya Abraham, kumetoa fursa ya kistratijia kwa ajili ya Marekani kushirikiana kwa karibu na washirika wake wakuu dhidi ya vitisho vya pamoja katika eneo la Mashariki ya Kati.

Inaonekana kuwa matukio ya hivi karibuni ambayo yamepelekea baadhi ya nchi za Kiarabu ambazo ni Imarati, Bahrain, Morocco na Sudan kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni yamechangia pakubwa katika lengo kuu la utawala wa Trump la kubuni muungano wa uhasama dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na vilevile mrengo wa mapambano ya Kiislamu kwa ushirikiano wa utawala haramu wa Israel na waitifaki wa Marekani na hivyo kupelekea serikali ya Washington kufanya mabadiliko hayo muhimu ya kistratijia katika mfumo wake wa kijeshi kuhusu eneo la Asia Magharibi.

CENTCOM

Kutolewa Israel katika mfumo wa kijeshi wa Marekani wa eneo la Ulaya na kuingizwa katika eneo la kamandi kuu ya kigaidi ya Marekani CENTCOM, bila shaka kutarahisisha ushirikiano wa kamandi hiyo na Utawala wa Israel na vilevile washirika wa Kiarabu wa Marekani Asia Magharibi kwa lengo la kutekeleza vitendo vya kigaidi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Huku ikisisitiza kuwa Israel ni mshirika wa kistratijia wa Marekani, Pentagon imesema kuwa mabadiliko hayo ya kamandi ya kijeshi yataimarisha zaidi ushirikiano wa CENTCOM na washirika wa Marekani na wakati huo huo kuboresha uhsirikiano wa Israel na washirika wa Ulaya wa Marekani.

Baada ya nchi saliti za Kiarabu kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa Tel Aviv, lobi za Kizayuni nchini Marekani zimekuwa zikiiomba serikali ya Trump iuweke utawala huo katika kamandi kuu ya CENTCOM. Moja ya lobi hizo ni lobi ya Jewish Institute for National Security of America ambayo Disemba iliyopita ilimtaka Trump aiweke Israel katika kamandi hiyo kwa hoja kuwa hatua hiyo itaimarisha ushirikiano kati ya Tel Aviv na nchi za Kiarabu dhidi ya Iran.

Kwa mujibu wa Martin Indyk, mwanachama wa taasisi ya Baraza la Uhusiano wa Kigeni la Marekani, kwa kutilia maanani kwamba masuala yanayohusiana na Iran yamebadilika na kuwa chanzo cha wasiwasi mkubwa kwa utawala wa Israel na baadhi ya nchi za Kiarabu, ushirikiano wa Tel Aviv na CENTCOM ni jambo la kimantiki na hatua nzuri.

Manuva ya Iran kulinda usalama katika maji ya Ghuba ya Uajemi

Inaonekana kuwa kwa hatua hiyo, Marekani inakusudia kuendesha moja kwa moja mashinikizo dhidi ya Iran na mrengo wa mapambano ya Kiislamu kwa ushirikiano wa nchi za Kiarabu na utawala haramu wa Israel. Ni wazi kuwa kushindwa mara kwa mara kwa mbinu za Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu zikiwemo za mashinikizo ya juu kabisa na vitisho visivyokoma vya kijeshi, kumeipelekea nchi hiyo kubuni muungano wa nchi za Kiarabu na Kizayuni kwa madhumuni ya kujaribu tena kufikia lengo hilo la kuifanya Iran isalimu amri mbele ya matakwa yake haramu na ya kibeberu.

Katika uwanja huo, inaonekana kuwa sasa hatua zote za pamoja za kijeshi na habari za usalama na kijeshi za utawala wa Kizayuni na nchi za Kiarabu dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran zitakuwa zikisimamiwa na kuendeshwa moja kwa moja kupitia CENTCOM. Pamoja na hayo lakini Iran imethibitisha kivitendo kuwa haitishwi na vitisho vyovyote vya Marekani bali itakabiliana vilivyo na njama zozote zitakazofanywa na vibaraka wa Marekani katika eneo.

Tags