Jan 18, 2021 11:22 UTC
  • Wapalestina wakaribisha tangazo la tarehe ya kufanyika uchaguzi mkuu

Mahmoud Abbas, Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina ametangaza kwamba uchaguzi mkuu wa bunge na rais wa mamlaka hiyo utafanyika katika hatua tatu tofauti. Amesema uchaguzi wa bunge utafanyika tarehe 22 Mei, wa rais Julai 31 na wa mabaraza ya miji tarehe 31 Agosti mwaka huu.

Kutangazwa tarehe ya kufanyika uchaguzi mkuu wa Palestina ni hatua muhimu katika mfumo wa kisiasa wa taifa hilo. Uchaguzi mkuu wa mwisho wa rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina ulifanyika mwaka 2005 ambapo Mahmoud Abbas alichaguliwa kuchukua nafasi ya Yassir Arafat. Uchaguzi wa rais ulioainishwa kufanyika tarehe 31 Julai una umuhimu mkubwa kwa kutilia maanani kwamba huenda mtu mwingine akachaguliwa kuchukua nafasi ya Mahmoud Abbas aliye na umri wa miaka 85.

Uchaguzi wa mwisho wa bunge la Palestina pia ulifanyika mwaka 2006 na iwapo uchaguzi huo utafanyika tarehe 22 Mei kama ilivyotangazwa, utakuwa uchaguzi wa kwanza wa bunge kufanyika baada ya kupita miaka 15. Bunge hilo lina viti 132. Umuhimu wa uchaguzi huo ni kwamba kila chama kitakachoshinda na kuwa na wingi wa viti kitapewa fursa ya kuunda serikali ijayo. Chama cha Mapambano ya Kiislamu cha Hamas kilipata ushindi wa viti katika uchaguzi uliofanyika 2006 na kikafanikiwa kuunda serikali lakini mwaka uliofuata wa 2007 vita vya ndani vilizuka, serikali ikavunjwa na na kwa mara nyingine chama cha Fat'h kikachukua madaraka.

Mahmoud Abbas akitangaza tarehe ya uchaguzi wa Palestina

Hivi sasa serikali inayotawala Palestinam haiungwi mkono na makundi ya kisiasa yaliyo katika Ukanda wa Gaza na inahitilafu nyingi za kisiasa na kiusalama na ukanda huo. Suala lenye umuhimu mkubwa hapa ni kwamba baadhi ya wajuzi wa mambo wanasema kuwa iwapo Hamas itashinda tena katika uchaguzi huo, huenda hitilafu za kisiasa zikaibuliwa tena kati ya makundi ya Palestina na hivyo kutopewa fursa ya kubuni serikali ya baadaye ya Palestina. Hilo ni jambo ambalo linawezekana kabisa kwa kutilia maana kuwa utawala haramu wa Israel unafanya uchochezi mkubwa katika uwanja huo kwa madhara ya chama cha Hamas.

Pamoja na hayo, lakini nafsi ya kutangazwa tarehe ya kufanyika uchaguzi mkuu huko Palestina inahesabiwa kuwa hatua nzuri. Ni kutokana na ukweli huo ndipo Hamas na Fat'h zote zikaunga mkono hatua hiyo iliyochukuliwa na Mahmoud Abbas. Huku ikisifu hatua hiyo, Hamas imesema kuwa ina hamu kubwa ya kuona kuwa haki hiyo ya taifa la Palestina inafikiwa. Nayo Fat'h imesema hatua hiyo ya Mahmoud Abbas ni nzuri na kwamba itapelekea kufikiwa azma ya watu wa Palestina.

Kukaribishwa kwa hatua hiyo ya Mahmoud Abbas kunaweza kutathminiwa kwa mitazamo miwili tofauti. Wa kwanza ni kuwa, kutangazwa tarehe ya kufanyika uchaguzi mkuu kuna maana ya kuafikiana makundi ya Palestina kwa madhumuni ya kubuni serikali na bunge la taifa hilo. Ni kutokana na ukweli huo ndipo Osama al-Qawasimi, Msemaji wa Fat'h akasema kuwa watu wa Palestina sasa wanapitia kipindi muhimu na cha kihistoria kwa ajili ya kumaliza mifarakano ambayo imedumu baina yao kwa miaka 13. Jambo la pili ni kuwa Kutangazwa tarehe ya kufanyika uchaguzi huo mkuu ni radiamali ya moja kwa moja dhidi ya mipango ya kisaliti ambayo imechukuliwa na baadhi ya nchi za Kiarabu kwa madhumuni ya kuwa na uhusiano wa kawaida na utawala ghasibu wa Israel kwa madhara ya taifa la Palestina.

Nembo za vyama vya Fat'h (kushoto) na Hamas

Nukta ya mwisho na muhimu ni kwamba uchaguzi huo unafanyika katika maeneo ya Quds Mashariki, Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na Ukanda wa Gaza. Kwa maana kwamba Wapalestina hawajakubali mpango wa hiana wa 'Muamala wa Karne', uliobuniwa na Marekani kwa ushirikiano wa nchi kadhaa saliti za Kiarabu, na wangali wanasisitiza juu ya Palestina kuendelea kudhibiti eneo la Quds Mashariki. Kufanyika uchaguzi katika eneo hilo la kijografia pia kunaweza kuchukuliwa kuwa ni suhindi mkubwa kwa Wapalestina.

Tags