Jan 19, 2021 02:35 UTC
  • Jumbe za kimataifa za kupinga tuhuma za ugaidi za Marekani dhidi ya Ansarullah ya Yemen

Hivi karibuni Mike Pompeo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani alitangaza kuwa serikali ya Rais Donald Trump imeijulisha rasmi Congress ya nchi hiyo kuwa imeliweka kundi la mapambano ya Kiislamu la Ansarullah la nchini Yemen katika orodha ya makundi yanayotuhumiwa kuunga mkono ugaidi, uamuzi ambao umekabiliwa na upinzani mkali wa kimataifa.

Uamuzi huo haujapingwa ndani ya Yemen na eneo la Asia Magharibi tu bali umekabiliwa na ipinzani mkali wa maeneo mengine mengi ya dunia. Umoja wa Ulaya umepinga uamuzi huo na kusema umezua wasiwasi mkubwa katika ngazi za kimataifa. Jambo hilo limekabiliwa na upinzani pia ndani ya Marekani kwenyewe ambapo wabunge 25 wa Congress wakiongozwa na Gregory Meeks, Mwenyekiti wa Kamati ya Masula ya Kigeni, wamelaani hatua ya Trump ya kuituhumu Ansarullah kuwa ni kundi la kigaidi.

Ni kwa nini kukawa na radiamali yote hiyo kubwa kimataifa? Je, Ulaya na baadhi ya Wamarekani wanaunga mkono Ansarullah mkabala na muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia huko Yemen? Bila shaka hapana. Lengo la Ulaya na baadhi ya Wamarekani sio kuunga mkono Ansarullah dhidi ya muungano huo wa Saudia.

Moja ya sababu za upinzani huo mkali dhidi ya uamuzi wa utawala wa Trump wa kulituhumu kundi la Ansarullah kuwa ni kundi la kigaidi ni kutokana na hali ya kutisha ya kibinadamu inayotawala huko Yemen. Kutuhumiwa Ansarullah kuwa ni kundi la kigaidi hakusaidii lolote katika kupunguza mgogoro wa kibinadamu wa Yemen bali kunavuruga zaidi juhudi za kisiasa za kujaribu kupunguza mgogoro huo. Ujumbe usio wa moja kwa moja wa maudhui hiyo ni kuwa Ansarullah imekubalika rasmi kuwa moja ya makundi muhimu ya kisiasa katika uwanja wa siasa za Yemen na hivyo kuitengwa katika mazungumzo yoyote ya kisiasa kutavuruga utatuzi wa aina yoyote wa kisiasa wa mgogoro huo.

Gregory Meeks

Sababu nyingine ni kuwa hata kama kufikia sasa Umoja wa Mataifa umeshindwa kutatua mgogoro wa Yemen, lakini hatua ya Marekani ya kuituhumu Ansarullah kuwa ni kundi la kigaidi itavuruga kabisa juhudi za Umoja wa Mataifa kushughulikia masuala ya nchi hiyo ya Kiarabu. Katika mazingira ya sasa pia, Serikali ya Wokovu wa Kitaifa ya Yemen na viongozi wa Ansarullah wamekuwa wakiutuhumu Umoja wa Mataifa kuwa unashughulikia maslahi ya Saudi Arabia na Imarati katika nchi hiyo kwa madhara ya watu wa Yemen.

Muhammad Abdussalaam, mkuu wa ujumbe wa mazungumzo wa Serikali ya Wokovu wa Kitaifa aliandika kupitia ujumbe wa mtandao wa kijamii wa Twitter kwamba: 'Martin Griffiths, mjumbe wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia msuala ya Yemen amekuwa na utendaji mbaya na kuunga mkono serikali kibaraka pamoja na kukubali malengo na mantiki yake, na hivyo kupuuza majukumu yake ya kimataifa kuhusu Yemen. Amebadilika na kuwa muhudumu wa idara ya posta ya Riyadh na Abu Dhabi kwa ajili ya kuwapatanisha vibaraka wanaohasimiana kati ya pande mbili hizo.'

Gregory Meeks, Mwenyekiti wa Kamati ya Masula ya Kigeni ya Congress ya Marekania pia amesema katika upinzani wake dhidi ya hatua hiyo ya Trump kwamba: Hatua hiyo inafanya kuwa ngumu zaidi kazi ya Martin Griffiths, akiwa mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa katika mazungumzo ya amani ya Yemen na hivyo kuweka vizingiti katika njia ya kumaliza vita hivyo. Kwa hakika ujumbe wa moja kwa moja wa maudhui hiyo ni kuufanya Umoja wa Mataifa uonekane kuwa umeshindwa katika utatuzi wa mgogoro wa Yemen.

Sababu ya tatu ya kupingwa uamuzi wa Marekani wa kuliweka kundi la Ansarullah katika orodha ya makundi ya kigaidi, ni kuwa uamuzi huo una maana ya moja kwa moja ya kutangazwa rasmi uungaji mkono wa Marekani kwa muungano wa kijeshi wa Saudia katika vita vyake dhidi ya Yemen. Katika miaka sita iliyopita muungano huo umehusika na kashfa na jinai kubwa za kibinadamu dhidi ya watu wa Yemen. Ushahidi uliopo unathibitisha wazi kwamba Marekani imeshiriki kwa njia za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja katika jinai hizo kutokana na msaada wake mkubwa wa silaha na kifedha kwa muungano huo.

Maandamano ya kupinga jinai za Marekani na Saudia nchini Yemen

Uamuzi wa Marekani wa kuiweka Ansarullah katika orodha ya makundi ya kigaidi umeifurahisha sana Saudia, na hata inasemekana kuwa ni nchi hiyo ya Kiarabu ndiyo iliupa utawala wa Trump ambao uko katika siku zake za mwisho za utawala, pendekezo la kuwekwa Ansarullah katika orodha hiyo. Suala hilo pia lina jumbe mbili. Ujumbe wa kwanza ni kuwa kuanzia sasa Marekani haitaunga tena muungano wa kijeshi wa Saudia dhidi ya Yemen na wa pili ni kuwa kutuhumiwa Ansarullah kuwa kundi la kigaidi unatoa mwanya mwingine kwa Saudia kutekeleza kila aina ya jinai dhidi ya watu wa Yemen kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi.

Nukta ya mwisho ni kwamba upinzani mkali wa kimataifa dhidi ya uamuzi wa Trump wa kuiweka Ansarullah katika makundi ya kigaidi ni kushindwa kwingine kwa utawala wa Trump katika siasa zake za kigeni, utawala ambao umebakia na siku moja tu ya kutawala Marekani kwa kutilia maani kuwa utasahaulika na kuwekwa kwenye historia kuanzia siku ya Jumatano, lakini pamoja na hayo jinai zake kubwa na hasa dhidi ya mataifa ya Asia Magharibi hazitasahaulika milele.

 

Tags