Jan 19, 2021 08:02 UTC
  • Qatar yazitaka nchi za Kiarabu za Ghuba ya Uajemi zifanye mazungumzo na Iran

Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar amezitaka nchi za Kiarabu za eneo la Ghuba ya Uajemi zifanye mazungumzo na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Sheikh Muhammad Abdurahman Al Thani amesema, kwa muda mrefu amekuwa akitaka kifanyike kikao cha mazungumzo kati ya wakuu wa nchi za Kiarabu za eneo la Ghuba ya Uajemi na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na angependa ashuhudie mwafaka juu ya suala hilo unafikiwa.

Kuhusu mvutano uliopo kati ya nchi yake na Imarati, waziri wa mambo ya nje wa Qatar amesema, kungali kuna safari ndefu hadi kutatuliwa tofauti zilizopo baina ya nchi yake na Imarati.

Viongozi waandamizi wa Imarati walisikika hivi karibuni wakidai kuwa, kumalizwa kikamilifu tofauti zilizopo kati ya nchi hiyo na Qatar kutategemea pia jinsi Qatar itakavyojikurubisha au kujiweka mbali na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Hivi karibuni Qatar ilitatua mgogoro wa kidiplomasia uliokuwepo baina yake na Saudi Arabia, Bahrain, Imarati na Misri ambao ulidumu kwa muda wa zaidi ya miaka mitatu.

Itakumbukwa kuwa mwezi Juni 2017, Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu, Bahrain na Misri, zilivunja uhusiano wao wa kiuchumi na kidiplomasia na Qatar kwa kuituhumu pamoja na mambo mengine nchi hiyo kwamba inafadhili ugaidi na kuwa na ukuruba na Iran, tuhuma ambazo Doha ilizikanusha. Nchi hizo ziliiwekea pia Qatar vikwazo vya anga, nchi kavu na baharini.../

Tags