Jan 19, 2021 11:23 UTC
  • Chanjo ya COVID-19 yaanza kutolewa kwa wakimbizi nchini Jordan

Wakimbizi nchini Jordan wameanza kupigwa chanjo ya COVID-19 ikiwa ni sehemu ya mpango wa kitaifa wa afya ambao unajumuisha raia wote, wakimbizi na wakazi.

Wakimbizi 43 kutoka kambi ya wakimbizi ya Al-Zaatari wamepatiwa chanjo hiyo katika katika kituo cha magonjwa kilichoko Mafraq, mji ulioko karibu na kambi hiyo. Mipango ya wengine zaidi kuchanjwa inaendelea. 

Shirika la la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR, limekuwa likisaidia juhudi za serikali ya Jordan ambayo kupitia wizara yake ya afya imezindua kampeni ya chanjo katika vituo 29 vya afya kote nchini.  

UNHCR imekuwa ikisaidia katika kuhamasisha na kusaidia wakimbizi kujiandikisha kwa ajili ya kudungwa chanjo na pia kwa kuwapatia usafiri wa kufika kwenye kiliniki za afya pale inapohitajika.  

Zaidi ya watu 200,000 wamesajiliwa katika mfumo wa serikali; na UNHCR hivi sasa inafahamu kuwa wakimbizi 53 wameshapewa miadi ya kuchanjwa.

Kama sehemu ya mpango wa kitaifa wa chanjo ya COVID-19 ya nchi hiyo, mtu yeyote anayeishi kwenye ardhi ya Jordan, pamoja na wakimbizi na wanaotafuta hifadhi, anastahili kupatiwa chanjo hiyo bila malipo. 

UNHCR imesema, inaendelea na kampeni katika ngazi za nchi, kikanda na ulimwengu mzima kuhakikisha wakimbizi na watu wengine inaowalinda wanajumuishwa katika mikakati ya kitaifa. Aidha kuhakikisha, kama ni kipaumbele, chanjo zinapatikana kwa walio hatarini zaidi kama wazee, wale walio na magonjwa sugu au watu ambao wana kinga ndogo, pamoja na wafanyakazi wa sekta ya afya na wengine walio na kazi muhimu za kimfumo. 

Jordan ambayo imewapatia hifadhi wakimbizi wapatao 750,000 waliosajiliwa na UNHCR, ilianzisha hatua kali zaidi wakati wa kipindi cha mwanzo cha janga la virusi vya corona katika jaribio la kuzuia kuenea kwa virusi. 

Idadi ya wakimbizi ambao walikutwa na virusi vya COVID-19 nchini Jordan imebaki kuwa ya chini kwa asilimia 1.6, ikilinganishwa na asilimia tatu miongoni mwa raia wa Jordan.../