Jan 19, 2021 11:26 UTC
  • Israel yaishurutisha Uturuki iifunge ofisi ya HAMAS ili kurejesha uhusiano kamili

Gazeti moja la Kiebrania limeripoti kuwa, utawala wa Kizayuni wa Israel umetoa sharti kwa Uturuki la kuifunga ofisi ya HAMAS mjini Istanbul ili kuanzisha tena uhusiano kamili na nchi hiyo.

Gazeti la Kizayuni ya Yediot Ahronot limeandika kuwa, utawala wa Kizayuni umetoa masharti mengi kwa ajili ya kurejesha tena uhusiano wa kawaida na Uturuki, lakini lililo wazi zaidi ni kutaka Ankara iahidi kuifunga ofisi ya Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS iliyoko mjini Istanbul na kusimamisha shughuli za mateka Wapalestina walioachiwa huru ambao wana mfungamano na brigedi za Izzuddin al-Qassam, tawi la kijeshi la Hamas.

Hivi karibuni wizara ya mambo ya nje ya utawala wa Kizayuni ilimteua balozi wake wa Bulgaria Irit Lillian kuwa balozi mpya wa utawala huo haramu nchini Uturuki.

Karibu mwezi mmoja nyuma, vyombo vya habari vya utawala wa Kizayuni vilidai kuwa, Rais Ilham Aliyev wa Jamhuri ya Azerbaijan anafanya juhudi za kuupatanisha utawala wa Kizayuni wa Israel na Uturuki ili kurejeshwa uhusiano kamili baina ya pande hizo mbili.

Rais Recep Tayyip Erdogan naye pia amenukuliwa akisema kuwa nchi yake inataka kuwa na uhusiano mzuri zaidi na utawala wa Kizayuni lakini sera za utawala huo kuhusiana na Palestina zinakwamisha suala hilo.../

Tags