Jan 20, 2021 07:51 UTC
  • Spika wa Bunge la Kuwait: Nchi yetu inapinga kuanzishwa uhusiano wa kawaida na Israel

Spika wa Bunge la Kuwait amesisitiza kwa mara nyingine tena kwamba, msimamo wa nchi yake kuhusiana na Palestina uko thabiti na si wenye kubadilika na kwamba, nchi hiyo inapinga kuanzishwa uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel.

Marzouq Ali Mohammed Al-Ghanim, Spika wa Bunge la Kuwait amesema hayo katika mazungumzo yake na Jibril Rajoub, Katibu wa Kamati Kuu ya Harakati ya Fat'h ya Palestina na kubainisha kwamba, nchi yake itaendelea kuiunga mkono Palestina na haitaingia katika mkumbo wa kuanzisha uhusiano wa kawaida na Israel.

Aidha amesisitiza kuwa, uvamizi na ukaliaji mabavu wa ardhi za Palestina unapaswa kuhitimishwa na kwamba, Kuwait inakaribisha kwa mikono miwili suala la umoja wa kitaifa wa Palestina na kufanyika uchaguzi wa Bunge na Rais huko Palestina.

Hivi karibuni Amir mpya wa Kuwait, Nawaf Al-Ahmad Al-Jaber Al-Sabah alisema kuwa, msimamo wa nchi yake kuhusiana na kadhia ya Palestina katika duru na majukwaa ya kimataifa uko thabiti na si wenye kubadilika.

Mawaziri wa Mashauri ya Kigeni wa Imarati na Bahrain wakionyesha nyaraka baada ya kutiliana saini na Israel hati ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala huo ghasibu kwa usimamizi wa Marekani

 

Kuwait imekuwa ikisisitiza mara kwa mara juu ya msimamo wake thabiti na usiotetereka kuhusiana na kadhia ya Palestina pamoja na haki za wananchi hao madhulumu huku ikiunga mkono kuundwa nchi huru ya Palestina mji mkuu wake ukiwa Baitul-Muqaddas.

Morocco ndio nchi ya karibuni kabisa ya Kiarabu kuanzisha uhusiano na Israel. Mbali na Morocco, nchi zingine za Kiarabu ambazo zimeanzisha uhusiano na Israel ni pamoja na Imarati, Bahrain na Sudan ambazo zimeanzisha uhusiano na utawala huo dhalimu katika fremu ya njama za Marekani-Kizayuni za kudhoofisha uungaji mkono wa nchi za Kiarabu kwa harakati za kupigania ukombozi wa Palestina. 

Tags