Jan 20, 2021 09:20 UTC
  • Radiamali na sababu za pendekezo la kuakhirishwa uchaguzi wa bunge nchini Iraq

Tume ya Uchaguzi nchini Iraq imetaka kuakhirishwa kwa miezi minne uchaguzi wa bunge wa nchi hiyo na badala ya kufanyika mwezi Juni, uitishwe mwezi Oktoba mwaka huu wa 2021.

Ilikuwa imepangwa kuwa, uchaguzi wa kabla ya wakati wake ufanyike tarehe 6 Juni, 2021. Hata hivyo hadi hivi sasa serikali ya Iraq haijatangaza msimamo wake wa mwisho kuhusu kuakhirishwa uchaguzi huo hadi mwezi Oktoba mwaka huu.

Makundi ya kisiasa nchini Iraq hayana kauli moja kuhusu kuakhirishwa uchaguzi huo. Kwa mfano muungano wa al Fat'h unapinga kuchereweshwa uchaguzi huo. Hoja zinazotolewa na muungano huo ni kwamba kusogezwa mbele tarehe ya uchaguzi huo ni kinyume na makubaliano ya Serikali na makundi ya kisiasa ya kuitishwa uchaguzi mpya katika kipindi cha mwaka mmoja tangu kuundwa serikali hiyo. Ukweli ni kuwa moja ya masharti aliyowekewa Waziri Mkuu wa Iraq, Mustafa al Kadhimi katika kikao cha kuomba imani ya wabunge, ni kuitisha uchaguzi wa mapema wa bunge, mwaka mmoja baada ya kuunda serikali yake.

Mustafa al Kadhimi

 

Muungano wa Vikosi vya Iraq unaoongozwa na Muhammad al Halbousi, Spika wa Bunge la Iran ambaye kimsingi lazima atoke kati ya Waislamu wa Kisuni wa Iraq, nao unapinga kupigwa kalenda uchaguzi huo. Hoja zilizotolewa na muungano huo ni kwamba sasa Serikali kupitia tume ya uchaguzi inataka kutia ulimi puani na kwenda kinyume na ahadi zake kwa makundi ya kisiasa ya kuitisha uchaguzi wa Bunge mwaka mmoja baada ya kuundwa serikali hiyo. Muungano huo unasema, hakuna dhamana yoyote ya kuitishwa uchaguzi huo hata huo mwezi Oktoba. Msimamo huo wa muungano wa Spika wa Bunge la Iraq unaashiria wazi wasiwasi wake kwamba, Serikali haina nia ya kuitisha uchaguzi huo.

Huku muungano wa Sadr ukiwa haujatangaza msimamo wa wazi kuhusu kuakhirishwa uchaguzi huo, muungano wa Hikmat wa Ammar al Hakim umeunga mkono kusogezwa mbele uchaguzi huo wa Bunge. Muungano huo unatoa sababu mbili za kukubaliana na suala hilo. Sababu ya kwanza ni kwamba, inaonekana katika uchaguzi ujao, muungano wa Ammar al Hakim utaungana na ule wa Mustafa al Kadhimi ili kuwa na viti vingi bungeni. Ni kwa sababu hiyo ndio maana bila ya kusita muungano wa Hikmat umeunga mkono pendekezo la tume ya uchaguzi la kuakhirisha uchaguzi huo. Sababu ya pili ni kwamba muungano huo wa Ammar al Hakim unaamini kuwa katika kipindi cha mwaka mmoja, kumejitokeza makundi mapya ya kisiasa na mwaka mmoja hautoshi kuelewa kwa kina undani wa makundi hayo. Hivyo kama uchaguzi utasogezwa mbele, makundi ya kisiasa nchini Iraq yatapata fursa zaidi ya kuyachunguza makundi hayo mapya na kujua ni lipi la kuungana nalo.

Uchaguzi nchini Iraq

 

Nukta nyingine ya kuizingatia hapa ni kwamba, makundi ya kisiasa ya Kikurdi, hadi hivi sasa hayajatoa msimamo wowote kuhusu suala hilo. Baadhi ya makundi makuu ya Kisuni nayo hadi hisi sasa yamenyamaza kimya. Yote haya yanaonesha kwamba, hakuna msimamo mmoja ndani ya Iraq kuhusu kuakhirishwa uchaguzi huo.

Amma tukija katika swali la kwa nini kuna uwezekano serikali ya Iraq ikakubaliana na pendekezo la kusogezwa mbele kwa miezi minne uchaguzi wa bunge, tunaweza kusema kwamba, sababu ya kwanza ni kuwa, Serikali haina fedha za kugharamia uchaguzi huo mwezi Juni. Hivi sasa Iraq inapambana na matatizo mengi ya kifedha, matatizo ambayo hivi karibuni pia yalisababisha maandamano makubwa ya kupinga serikali na kulalamikia matatizo ya kiuchumi. Sababu ya pili ni ile iliyotajwa na tume ya uchaguzi ya nchi hiyo kwamba muda wa kujiandikisha umemalizika na miungano michache tu ya kisiasa ndiyo iliyojiandikisha kushiriki katika uchaguzi huo. Hivyo kuna ulazima wa kusogezwa mbele tarehe ya uchaguzi huo ili kutoa fursa kwa makundi yote kufaidika na haki yao hiyo ya kidemokrasia. 

Kwa kumalizia ni vyema tuseme kwamba, ndani ya Bunge la Iraq pia, baadhi ya makundi yanapingana na msimamo wa Spika wa bunge hilo na hayaoni busara kufanyika uchaguzi mwezi Juni mwaka huu yakiaini kwamba watu wengi watakosa haki yao ya kupiga kura.

Tags