Jan 20, 2021 12:05 UTC
  • Indhari ya makundi ya muqawama ya Palestina kwa utawala wa Kizayuni

Makundi ya muqawama katika Ukanda wa Ghaza yamesema kuwa umoja ni njia pekee ya kukabiliana na njama za utawala wa Kizayuni dhidi ya kadhia ya Palestina.

Makundi ya muqawama ya Palestina leo Jumatano yameitisha kikao na kueleza kuwa umoja wa kitaifa ni njia pekee ya uhakika kwa ajili ya kukabiliana na njama zilizoratibiwa kwa lengo la kuisambaratisha kadhia ya Palestina. 

Makundi hayo ya muqawama ya Palestina yamesisitiza pia udharura wa kufanyika mazungumzo mapana ya kitaifa ya makundi yote ya Palestina kabla ya kuanza uchaguzi na kueleza kuwa: Mazingira yanapaswa kuandaliwa ili kufanikisha mchakato wa uchaguzi; ikiwemo kuiondolea Ghaza vikwazo na kuwarejeshea haki zao wafanyakazi na familia za mateka wa Kipalestina. 

Makundi ya muqawama ya Palestina yametangaza kuwa, mashambulizi ya utawala wa Kizayuni katika mji wa Quds na kuendelea utawala huo kuchimba chini kwa chini karibu na msikiti mtukufu wa al Aqsa ni hatari kuu inayohitajia jitihada za nchi za Kiarabu na Kiislamu ili kuunusuru msikiti huo mtukufu.

Mashambulizi ya Wazayuni katika msikiti wa al Aqsa  

Makundi ya mapambano ya Palestina yamewatahadharisha maghasibu wa Kizayuni juu ya kuendeleza siasa zao za kihasama mkabala na haki ya wananchi wa Palestina na matukufu yao na kusisitiza kuwa yako bega kwa bega na wafungwa wa Kipalestina khususan katika kipindi hiki ambapo jela za utawala wa Kizayuni zimelemewa na maambukizi ya corona. 

Tags