Jan 21, 2021 07:27 UTC
  • Kwa siku moja tu, mateka 41 Wapalestina wameambukizwa corona katika jela za Israel

Maafisa wa Palestina wamesema, mateka 41 wameambukizwa virusi vya corona ndani ya muda wa siku moja katika jela za utawala haramu wa Kizayuni wa Israel wanakoshikiliwa.

Klabu ya mateka Wapalestina imetangaza kuwa, jana Jumatano mateka 41 walioko kwenye jela za Raymun na An-Naqb walibainika kuwa na virusi vya corona vinavyosababisha maradhi ya Covid-19.

Asasi hiyo ya Palestina imeongeza kuwa, kutokana na maambukizo hayo, idadi ya mateka Wapalestina walioambukizwa virusi vya corona wakiwa kwenye magereza ya utawala wa Kizayuni imeongezeka na kufika 290.

Tangu ulipozuka mripuko wa virusi vya corona, zimekuwa zikitolewa ripoti kila mara zinazoonyesha jinsi maafisa wa utawala haramu wa Israel wasivyojali wala kuzipa uzito hali za kiafya za mateka Wapalestina wanaoshikiliwa kwenye magereza ya utawala huo.

Hivi karibuni, Idara ya habari inayohusika na masuala ya mateka Wapalestina ilitangaza kuwa, waziri wa usalama wa ndani wa utawala wa Kizayuni ameagiza mateka Wapalestina wa masuala ya usalama wasipigwe chanjo ya corona na kwamba chanjo hiyo itolewe kwa wafanyakazi tu wa magereza wanakoshikiliwa Wapalestina hao, uamuzi ambao unahalifu taratibu na hati za kimataifa.../

Tags