Jan 21, 2021 11:57 UTC
  • Iran yalaani milipuko ya kigaidi Baghdad, watu zaidi ya 28 wamepoteza maisha

Ubalozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran huko Baghdad Iraq umelaani mashambulizi ya kigaidi yaliyotekelezwa katika mji mkuu wa nchi hiyo na kuua shahidi na kujeruhiwa raia kadhaa wa nchi hiyo wasio na hatia.

Maidani ya al Tayran katikati mwa mji mkuu wa Iraq, Baghdad leo Alhamisi imeshuhudia milipuko miwili pacha ambapo kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na idara ya ulinzi wa raia ya Iraq watu 28 wamepoteza maisha na wengine 73 kujeruhiwa. 

Ubalozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran huko Baghdad umetoa taarifa ukitoa mkono wa pole kwa familia za wahanga wa jinai hiyo ya kigaidi na kuwatakia pia majeruhi wa milipuko hiyo shifaa ya haraka. Brigedia Jenerali Hazem al Azzawi Mkurugenzi wa Kamandi ya Oparesheni ya Baghdad ameliambia shirika la habari la Iraq (INA) kuwa, milipuko pacha imetokea katika soko lenye watu wengi katika eneo la Bab al Sharji karibu na maidani ya al Tayran.  

Milipuko pacha ya kigaidi huko Baghdad, Iraq, watu 28 wauawa 

Taarifa ya ubalozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran huko Baghdad aidha imeunga mkono hatua za serikali na vyombo vya usalama vya Iraq na kusisitiza kuwa: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kama ilivyo siku zote inasisitiza kuiunga mkono serikali na wananchi wa Iraq na iko tayari kutoa msaada wowote unaohitajika. 

Ubalozi wa Iran mjini Baghdad umesema unataraji kuwa vyombo vya usalama vya Iraq vitawatia nguvuni wahusika wakuu wa milipuko hiyo na kuwaadhibu.