Jan 22, 2021 03:55 UTC
  • Miripuko Iraq, muungano wa

Muungano wa "Daulat al Qanun" umelaani vikali miripuko ya kigaidi iliyotokea jana katika mji mkuu wa Iraq, Baghdad na kutaka kuangaliwa upya mipango na mikakati ya kulinda usalama wa maeneo yote ya nchi hiyo.

Hayo yameripotiwa na televisheni ya al Mayadeen ambayo imeunukuu muungano huo ukisisitiza kuwa, matukio ya kigaidi ya jana Alkhamisi, kwa mara nyingine yameonesha kwamba kuna udharura wa kuangaliwa upya mipango na mikakati ya ulinzi pamoja na kuwasaka magaidi wote wanaowakosesha amani wananchi wa Iraq.

Muungano huo aidha umeyataka makundi yote ya kisiasa nchini Iraq kuungana na kushirikiana katika kupambana na janga la ugaidi nchini humo. 

Huku hayo yakiripotiwa, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amelaani vikali miripuko miwili ya mabomu iliyotokea katika mji mkuu wa Iraq jana Alkhamisi na kuua shahidi na kujeruhi makumi ya watu wasio na hatia.

Magaidi kwa mara nyingine wameua watu wasio na hatia nchini Iraq

 

Saeed Khatibzadeh sambamba na kuelezea kusikitishwa kwake na mashambulio hayo ya kigaidi na kutoa mkono wa pole kwa wananchi na serikali ya Iraq, amesema, kama ilivyo siku zote, sasa hivi pia Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iko tayari kutoa msaada wowote unaohitajika na wakati wowote ule katika vita dhidi ya ugaidi na misimamo mikali.

Kabla ya hapo pia, Ubalozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran huko Baghdad Iraq nao ulikuwa umelaani mashambulizi hayo ya kigaidi.

Maidani ya al Tayran ya katikati mwa mji mkuu wa Iraq, Baghdad, jana Alhamisi ilikumbwa na miripuko miwili pacha illiyoua shahidi raia 32 wasio na hatia wa Iraq na kujeruhi wengine zaidi ya 100. 

Tags