Jan 22, 2021 08:18 UTC
  • Syria yasisitiza ulazima wa kuweko umoja kwa ajili ya kukabilianan na ugaidi

Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Syria imelaani mashambulio ya kigaidi yaliyotokea jana katika mji mkuu wa Iraq Baghdad na kusisitiza ulazima wa kuweko umoja na mshikamano wa kimataifa kwa ajili ya kupambana na ugaidi.

Taarifa ya Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Syria imeeleza kuwa, mashambulio haya ya kijinai kwa mara nyingine tena yameweka wazi ukweli huu kwamba, juhudi za kupambana na ugaidi haziwezi kuzaa matunda madhali ugaidi huo haujaangamizwa kikamilifu na hakujawa na umoja na mshikamano wa kimataifa kwa ajili ya vita hivyo.

Kadhaika taarifa ya Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Syria imebainisha kuwa, ugaidi ungali tishio kwa usalama na uthabiti wa kieneo na ulimwengu kwa ujumla.

Maidani ya al Tayran katikati mwa mji mkuu wa Iraq, Baghdad jana Alkhamisi ilishuhudia milipuko miwili pacha ambapo kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na idara ya ulinzi wa raia ya Iraq watu 32 wamepoteza maisha na makumi ya wengine kujeruhiwa. 

Usalama ukiwa umeimarishwa Baghdad baada ya shambulio la jana (21.01.2021) la kigaidi

 

Brigedia Jenerali Hazem al Azzawi Mkurugenzi wa Kamandi ya Oparesheni ya Baghdad ameliambia shirika la habari la Iraq (INA) kuwa, milipuko pacha imetokea katika soko lenye watu wengi katika eneo la Bab al Sharji karibu na maidani ya al Tayran.  

Mataifa na viongozi mbalimbali wa dunia sambamba na kutoa mkono wa pole kwa serikali, wananchi na familia za Iraq zilizopoteza ndugu na jamaa zao katika shambulio hilo la kigaidi, wamelaani vikali kitendo hicho cha kigaidi.

Tags