Jan 22, 2021 11:51 UTC
  • Waziri Mkuu wa Iraq: Magaidi wa Daesh (ISIS) wasubiri majibu makali ya jinai zao

Waziri Mkuu wa Iraq amesema kuwa, magaidi wa Daesh (ISIS) wasubiri majibu makali kutoka kwa wananchi na vikosi vya ulinzi vya nchi hiyo na kusisitiza kwamba serikali yake itahakikisha mashambulizi mengine ya kigaidi hayatokei nchini humo.

Vyombo vya habari vimemnukuu Mustafa al Kadhimi, Waziri Mkuu na Amirijeshi Mkuu wa Majeshi ya Iraq akisema hayo leo Ijumaa katika kikao cha dharura cha Baraza la Usalama wa Taifa la nchi hiyio na kuongeza kuwa, magaidi wametumia upenyo mdogo tu kufanya mashambulizi ya mabomu mjini Baghdad hivyo inabidi vipenyo kama hivyo viondolewe haraka.

Waziri Mkuu wa Iraq vile vile ametaka kutolewe mafunzo bora na kuongezwe uwezo na uimara wa vikosi vya ulinzi vya nchi hiyo akisisitiza kuwa, sasa hivi mji wa Baghdad unafanyia kazi mkakati mkubwa wa kiusalama na wenye taathira katika kukabiliana na changamoto zijazo za kiusalama na kwamba mkakati na stratijia hiyo inasimamiwe moja kwa moja na yeye mwenyewe Waziri Mkuu wa Iraq.

Magaidi wasio na chembe ya utu wameshambulia kigaidi na kiwoga wananchi wasio na hatia Iraq

 

Miongoni mwa nchi za kwanza kabisa kulaani mashambulizi ya jana ya kigaidi nchini Iraq ilikuwa ni Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambayo kupitia msemaji wake wa mambo ya nje Saeed Khatibzadeh na sambamba na kuelezea kusikitishwa kwake na mashambulio hayo ya kigaidi na kutoa mkono wa pole kwa wananchi na serikali ya Iraq, amesema, kama ilivyo siku zote, sasa hivi pia Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iko tayari kutoa msaada wowote unaohitajika na wakati wowote ule katika vita dhidi ya ugaidi na misimamo mikali.

Kabla ya hapo pia, Ubalozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran huko Baghdad Iraq nao ulikuwa umelaani mashambulizi hayo ya kigaidi.

Maidani ya al Tayran ya katikati mwa mji mkuu wa Iraq, Baghdad, jana Alkhamisi ilikumbwa na miripuko miwili pacha illiyoua shahidi raia 32 wasio na hatia wa Iraq na kujeruhi wengine zaidi ya 110. 

Tags