Jan 23, 2021 07:52 UTC
  • Yemen: Hakuna matumaini ya mabadiliko ya kimsingi katika siasa za Marekani

Mshauri wa Waziri Mkuu wa Yemen amesema kuwa, rais mpya wa Marekani, Joe Biden si mwokozi wa eneo hili tofauti kabisa na propaganda zinazopigwa. Amesema, hakuna matumaini ya kuweko mabadiliko ya kimsingi katika siasa za Marekani na kamwe Biden hatofanya kinyume na marais waliomtangulia wa nchi hiyo.

Hamid Abdul Qadir Antar amesema hayo usiku wa kuamkia leo katika mahojiano aliyofanyiwa na shirika la habari la IRNA na kuongeza kuwa, rais mpya wa Marekani aliahidi kwamba akishinda katika uchaguzi atakomesha mashambulizi ya kivamizi nchini Yemen na atafuta maamuzi yaliyochukuliwa na Donald Trump, lakini hakuna matumaini yoyote ya kutekelezwa ahadi hiyo kwani siasa za Marekani hazina tofauti hata kidogo na za utawala wa Kizayuni. Amesema, mabepari wa Kizayuni ndio waamuzi wakuu wa siasa za Marekani na kwamba marais wanaongia madarakani huko Marekani ni nyenzo tu za kufanikishia matakwa ya magenge yenye nguvu na mabepari wa nchi hiyo.

Rais wa Mareknai, Joe Biden

 

Kiongozi huyo wa ngazi za juu wa Yemen pia amesema, kitendo cha kiuadui cha Trump cha kuliingiza jina la Answarullah katika orodha yake ya makundi ya kigaidi hakitofanikiwa na hakina faida zaidi ya kuwaongezea mateso tu wananchi wa Yemen. Amesema, iwapo uadui huo wa Trump utatekelezwa, basi mlango wa mazungumzo na utatuzi wa kadhia ya Yemen utafungwa na haiwezekani kutatua mgogoro wa nchi hiyo bila ya kushirikishwa kikamilifu harakati ya wananchi ya Answarullah.

Katika siku za mwisho za serikali ya Donald Trump huko Marekani, waziri wa mambo ya nje wa nchi hiyo, Mike Pompeo, aliliingiza jina la Answarullah katika orodha ya kile kinachodaiwa na Washington kuwa ni makundi ya kigaidi hatua ambayo inaendelea kulaaniwa na hata na Umoja wa Mataifa na taasisi zake.

Tags