Jan 23, 2021 12:31 UTC
  • Wapakistani waandamana kupinga kuanzishwa uhusiano na Israel

Makumi ya maelfu ya wananchi wa Pakistan wamefanya maandamano ya kupinga uwezekano wowote wa kuanzishwa uhusiano kati ya nchi hiyo na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Maandamano hayo ya 'watu milioni moja' yaliyofanyika katika mji wa Karachi, yaliitishwa na Jumuiya ya Maulama wa Kiislamu wa Pakistan, Jamiat Ulema-i-Islam-Fazl (JUI-F).

Akizungumza katika maandamano hayo, Maulana Saleemullah Alwazi, Mkuu wa jumuiya hiyo ya wasomi wa Kiislamu nchini Pakistan ameeleza bayana kuwa, Israeli inahusika na mauaji ya kizazi ya Waislamu wa Palestina, na kwamba kamwe hawatairuhusu serikali ya federali (ya Pakistan) ianzishe uhusiano wa kidiplomasia na utawala huo.

Kadhalika wananchi wa Pakistan wametumia jukwaa la maandamano hayo kuonyesha uungaji mkono wao kwa wananchi madhulumu wa Palestina.

Serikali ya Pakistan mara kadhaa imesisitiza kuwa, kamwe haitoutambua utawala wa Kizayuni wa Israel licha ya mashinikizo ya nchi ajinabi.

Maanadamano ya wananchi wa Pakistan

Hivi karibuni, Shah Mahmood Qureshi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Pakistan ameuhutubu Umoja wa Falme za Kiarabu kwa kuuambia: Tumeweka wazi na tumeiambia bayana Imarati kuwa, kamwe Islamabad haitoitambua rasmi Israel hadi pale mgogoro wa Palestina utakapopatiwa ufumbuzi wa kudumu.

Kabla ya hapo pia, Waziri Mkuu wa Pakistan, Imran Khan alikanusha kuwepo mashinikizo ya aina yoyote ya kuitaka nchi hiyo ijiunge na safu ya nchi zinazofanya mapatano na utawala haramu wa Kizayuni wa Israel. Alisema wananchi wa Pakistan wako bega kwa bega na wananchi wa Palestina na wanawaunga mkono kikamilifu katika kuhakikisha wanarejeshewa haki zao.

Tags