Jan 24, 2021 09:54 UTC
  • Matamshi yenye mgongano ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudia kuhusu vita vya Yemen

Katika matamshi yanayoonyesha mgongano wa wazi, Faisal bin Farhan bin Abdullah, Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia amedai kwamba utawala wa Riyadh unataka kusimamisha vita vyake vya kichokozi dhidi ya Yemen na wakati huo huo kukaribisha hatua ya utawala ulioondoka madarakani wa Marekani ya kuituhumu Ansarullah kuwa ni kundi la kigaidi.

Karibu miezi mingine miwili ijayo vita vya Yemen vitaingia katika mwaka wake wa saba, vita ambavyo vimesababisha mgogoro mkubwa zaidi wa kibinadamu katika karne ya 21. Kuuawa zaidi ya Wayemen laki moja, kujeruhiwa mamia ya maelfu, watu karibu milioni 4 kulazimika kuishi kama wakimbizi na kuharibiwa miundomsingi ya nchi hiyo ni miongoni mwa matgokeo ya vita hivyo vya kichokozi vya Saudia dhidi ya Yemen.

Ni wazi kuwa matamshi hayo ya mgongano ya Faisal bin Farhan yanatokana na wasi wasi wa Saudia kuhusu kuendelea vita vya Yemen. Utawala wa Aal Saud ulianzisha vita katika kipindi cha uongozi wa Rais Barack Obama nchini Marekani na kudumisha vita hivyo vya jinai dhidi ya Wayemen wasio na hatia bila kuwa na woga wowote wa kukabiliwa na mashinikizo ya nje. Ni wazi kuwa Marekani ina mchango mkubwa katika maafa na jinai kubwa inayotekelezwa dhidi ya watu wa Yemen na kwa upande wa pili uungaji mkono wake wa wazi kwa jinai zinazotekelezwa na utawala wa Aal Saud dhidi ya taifa la Yemen umepelekea kutiliwa shaka madai yake ya eti kutetea thamani za kiutu na haki za binadamu duniani.

Ansarullah ya Yemen

Inaonekana kuwa serikali mpya ya Marekani imeamua kurekebisha sura nchi hiyo iliyochafuliwa na utawala wa Donald Trump na kwa msingi huo kuna uwezekano mkubwa wa kutazamwa upya siasa za Washington kuhusu vita vya Yemen. Tayari msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani ametangaza kuwa serikali mpya ya Rais Joe Biden imeanza kuchunguza tuhuma za kutajwa Ansarullah na serikali ya Trump kuwa ni kundi la kigaidi na kwamba uamuzi mpya unatazamiwa kuchukuliwa hivi karibuni kuhusu suala hilo.

Gary Sick Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Columbia na mwanachama wa zamani wa Baraza la Usalama wa Taifa la Marekani katika serikali tatu za Marais Jerald Ford, Jimmy Carter na Ronald Reagan amesema kwamba Joe Biden alipinga vikali vita dhidi ya Yemen na hivi sasa pia yuko mbioni kumaliza vita hivyo. Gary Sick amesisitiza kuwa iwapo Mrekani, Uingereza na Ufaransa zitakoma kutoa msaada wa kijeshi na kilohistiki kwa Saudi Arabia, bila shaka nchi hiyo ya kifalme hautakuwa na uwezo wa kudumisha kwa muda mrefu vita hivyo dhidi ya Yemen.

Kwa kutilia maanani matamshi hayo na uwezekano wa kubadilika siasa za Marekani kuhusu vita vya Yemen, Saudi Arabia ina wasi wasi mkubwa wa kuendeleza vita hivyo kwa kuhofia ongezeko la mashinikizo ya kimataifa dhidi yake, jambo ambalo limempelekea waziri wake wa mambo ya nje kutoa matamshi ya mgongano kuhusu vita hivyo.

Maudhui nyingine ni kwamba waziri huyo amedai kuwa muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudia dhidi ya Yemen haujazuia kusitishwa vita hivyo bali ni Ansarullah ndiyo inavuruga juhudi za kumalizwa vita hivyo ambavyo vimesababisha maafa makubwa dhidi ya nchi hiyo masikini. Wakati huo huo amekaribisha na kusifu hatua iliyochukuliwa katika siku za mwisho mwisho za utawala wa Trump za kuiweka Ansarullah katika orodha ya makundi yanayodaiwa na utawala wa Washington kuunga mkono ugaidi.

Gary Sick

Matamshi hayo ya Faisal bin Farhan yanathibitisha wazi kuchoshwa watawala wa Saudia na vita vya Yemen. Watawala hao wanaituhumu Ansarullah kuwa ndiyo imezuia kumalizika vita vya Yemen katika hali ambayo kundi hilo la Kiislamu limetekeleza mara kadhaa usitishaji vita uliofikiwa kufuatia mapatano ya Umoja wa Mataifa yakiwemo yale ya Disemba 2018 ya mjini Stockholm. Ni utawala wa Riyadh ndio unaozuia juhudi za kusimamisha vita hivyo kutokana na hatua zake za kukiuka mara kwa mara mapatano ya usitishaji vita, na hivyo kuilazimu Serikali ya Wokovu wa Kitaifa ya Yemen kujibu uchokozi wake.

Wakati huo huo, hatua ya Faisal bin Farhan ya kutetea kwa nguvu zake zote uamuzi wa Trump wa kuliweka kundi la Ansarullah katika orodha y makundi ya kigaidi inapingana wazi na madai yake ya kutaka kumaliza vita vya Yemen. Hii ni kwa sababu vita hivyo haviwezi kumalizika bila ya kushirikishwa Ansarullah katika juhudi za kuvimaliza na wakati huo huo kushirikishwa vilivyo katika muundo wa serikali ijayo ya Yemen.

Tags