Jan 24, 2021 13:52 UTC
  • Shambulio la DAESH dhidi ya Al-Hashdu-Sha'abi lilifanywa kwa msukumo na msaada wa Marekani

Chombo kimoja cha habari nchini Iraq kimetangaza kuwa, shambulio la magaidi wa kundi la ukufurishaji la DAESH (ISIS) dhidi ya wapiganaji wa Al-Hashdu-Sha'abi katika mkoa wa Salahuddin limefanywa kwa msukumo na msaada wa Marekani.

Jeshi la kujitolea la wananchi wa Iraq la Al-Hashdu-Sha'abi lilitangaza jana usiku kwamba wapiganaji wake 10 wameuawa shahidi katika shambulio lililofanywa na magaidi wa Daesh katika eneo la Hamrain mkoani Salahuddin kaskazini mwa nchi hiyo.

Shirika la habari la Al-A'had News limemnukuu afisa mmoja wa usalama ambaye hakutaka kutajwa jina lake na kuripti kuwa, mnamo siku chache nyuma kamera za kumurika taswira gizani za Al-Hashdu-Sha'abi zilinasa helikopta za kijeshi za askari vamizi wa Marekani zikitua kwenye eneo la milimani la Hamrain mkoani Salahuddin; na inavyoonekana helikopta hizo zilikuwa zimebeba misaada, silaha na vifaa vya kilojistiki kwa ajili ya makundi ya kigaidi.

Wapiganaji wa Al-Hashdu-Sha'abi baada ushindi dhidi ya Daesh

Afisa huyo wa usalama amesema, magaidi wa Daesh waliktumia silaha nzitonzito na za aina tofauti katika shambulio lao dhidi ya vikosi vya Al-Hashdu-Sha'abi huko Hamrain na akaongeza kuwa, vikosi vya jeshi la Marekani vingali vinatoa msukumo na msaada kwa magenge ya kigaidi ili yavuruge usalama na kuyadhibiti tena maeneo ya mkoa wa kaskazini wa Salahuddin.

Mnamo mwaka 2017 na baada ya miaka mitatu ya vita na mapigano, Iraq ilitangaza ushindi dhidi ya kundi la kigaidi na ukufurishaji la Daesh, lakini mabaki na vikundi vidogovidogo vya genge hilo vilivyotawanyika vingali vinaendesha harakati zao katika baadhi ya maeneo ya Iraq.

Hivi sasa vikosi vya usalama vya Iraq vinaendelea na operesheni kadhaa kwa madhumuni ya kuhakikisha magaidi hao wanatokomezwa kikamilifu katika ardhi ya nchi hiyo.../  

Tags