Jan 25, 2021 02:31 UTC
  • Hatua kali za kiusalama zachukuliwa katika mji mkuu wa Iraq, Baghdad

Duru moja ya Iraq imetangaza habari ya kuchukuliwa hatua kali za kiusalama katika mji mkuu wa nchi hiyo Baghdad hasa baada ya magaidi wa Daesh kufanya mashambulio ya kigaidi yaliyoua na kujeruhi makumi ya watu katikati ya mji huo Alkhamisi iliyopita.

Mtandao wa habari wa Shafaq News umeinukuu duru hiyo ya kuaminika ikisema kuwa, baada ya kupatikana taarifa za kiintelijensia kuhusu uwezekano wa kutokea shambulio jingine la kigaidi mjini humo, maafisa usalama wa Iraq wameamua kuweka ulinzi mkali kuanzia jana asubuhi.

Siku chache zilizopit, Waziri Mkuu wa Iraq alisema kuwa, magaidi wa Daesh (ISIS) wasubiri majibu makali kutoka kwa wananchi na vikosi vya ulinzi vya nchi hiyo na kusisitiza kwamba serikali yake itahakikisha mashambulizi mengine ya kigaidi hayatokei nchini humo.

Maidan ya al Tayran katikati ya Bagdad baada ya shambulio la kigaidi la tarehe 21 Januari, 2021

 

Vyombo vya habari vilimnukuu Mustafa al Kadhimi, Waziri Mkuu na Amirijeshi Mkuu wa Majeshi ya Iraq akisema hayo leo Ijumaa katika kikao cha dharura cha Baraza la Usalama wa Taifa la nchi hiyo na kuongeza kuwa, magaidi wametumia upenyo mdogo tu kufanya mashambulizi ya mabomu mjini Baghdad hivyo inabidi vipenyo kama hivyo viondolewe haraka.

Waziri Mkuu wa Iraq vile vile alitaka kutolewe mafunzo bora na kuongezwe uwezo na uimara wa vikosi vya ulinzi vya nchi hiyo akisisitiza kuwa, sasa hivi mji wa Baghdad unafanyia kazi mkakati mkubwa wa kiusalama na wenye taathira katika kukabiliana na changamoto zijazo za kiusalama na kwamba mkakati na stratijia hiyo inasimamiwe moja kwa moja na yeye mwenyewe Waziri Mkuu wa Iraq.

Maidani ya al Tayran ya katikati mwa mji mkuu wa Iraq, Baghdad, siku ya Alkhamisi ya tarehe 21 Januari, 2021 ilikumbwa na miripuko miwili pacha illiyoua shahidi raia 35 wasio na hatia wa Iraq na kujeruhi wengine zaidi ya 110. 

Tags