Jan 25, 2021 02:31 UTC
  • Wapalestina: Iran ndiye muungaji mkono mkuu wa ukombozi wa Palestina

Harakati ya Jihadul Islami ya Palestina imesema kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ndiye muungaji mkono mkuu wa ukombozi wa Palestina na muqawama wa taifa hilo mbele ya jinai za utawala wa Kizayuni.

Khadhr Adnan, mmoja wa viongozi waandamizi wa Jihadul Islami ya Palestina alisema hayo jana Jumapili wakati alipohojiwa na shirika la habari la FARS na kuongeza kuwa, kati ya umma wa Kiarabu na Kiislamu, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran daima ndiye muungaji mkono mkuu wa ukombozi wa Kibla cha Kwanza cha Waislamu yaani Msikti wa al Aqsa, mji wa Baytul Muqaddas, wananchi wanaodhulumiwa wa Palestina na maeneo mengine matukufu ya Palestina.

Amezungumzia pia hali mbaya ya mateka wa Kipalestina katika jela za kutisha za Israel na kulalamikia vikali kimya ya jamii ya kimataifa na taasisi zinazodai kutetea haki za binadamu duniani hasa wakati huu ambapo mateka hao wanataseka sana kwa ugonjwa wa COVID-19. Hivi sasa zaidi ya mateka 6,500 wa Kipalestina wanashikilishwa katika korokoro na jela za kuogofya za utawala wa Kizayuni wa Israel. 

Wanamapambano wa Jihadul Islami ya Palestina

 

Amma kuhusu umustakbali wa baadhi ya nchi za Kiarabu zilizotangaza uhusiano wao na utawala wa Kizayuni licha ya Israel kutenda jinai zisizo na kifani dhidi ya Wapalestina, kiongozi huyo mwandamizi wa Jihadul Islami ya Palestina amesema, watawala wa nchi hizo wanapaswa kutambua kwamba wameingia kwenye mtego mkubwa kwani lengo la utawala wa Kizayuni ni kupora tu utajiri wa nchi hizo. 

Hadi hivi sasa na kutokana na mashinikizo ya Marekani, nchi za Kiarabu za Imarati, Bahrain, Sudan na Morocco zimetangaza uhusiano wa kawaida na Wazayuni. Hata hivyo kitendo hicho kinaendelea kulaaniwa hadi leo hii na Waislamu kote ulimwenguni.

Tags