Jan 25, 2021 23:38 UTC
  • Sababu za kuongezeka mashambulio ya kigaidi ya ISIS nchini Iraq

Jana Jumatatu, Januari 25, 2021, Brigedia Jenerali Yahya Rasoul, msemaji wa Komandi Kuu ya Majeshi ya Iraq alizungumzia ushahidi mpya uliopatikana kuhusu mashambulio ya hivi karibuni ya mjini Baghdad na kusema kuwa, hadi hivi sasa vikosi vya usalama vya Iraq vimefanikiwa kuzima majaribio kadhaa makubwa ya kujiripua kwa mabomu katika maeneo tofauti ya nchi hiyo. 

Mabaki ya genge la kigaidi la Daesh (ISIS), Jumamosi usiku yalivamia na kushambulia kituo cha harakati ya kujitolea ya wananchi wa Iraq maarufu kwa jina la al Hashd al Sha'abi katika mkoa wa Salahuddin na kuua shahidi askari 11 wa harakati hiyo na kujeruhi wengine wanane.

Alkhamisi ya tarehe 21 Januari pia, Baghdad, mji mkuu wa Iraq ulikumbwa na miripuko miwili ya kujitolea muhanga kutoka kwa magaidi wa Daesh iliyoua watu 35 na kujeruhi wengine 110. Magaidi kutoka Saudi Arabia ndio waliohusika na mashambulizi hayo. Amma swali muhimu la kujiuliza hapa ni sababu gani zimepelekea kuongezeka mashambulio ya kigaidi nchini Iraq?

Nukta ya kwanza ni kwamba miripuko ya Bagdad na uvamizi wa mabaki ya magaidi wakufurishaji wa ISIS katika kituo cha al Hashd al Sha'abi huko Salahuddin ni mambo yaliyotokea baada tu ya kuingia madarakani rais mpya wa Marekani, Joe Biden. Matukio hiyo kwa namna fulani yamekusudia kutoa ujumbe kwa Washington kwamba Iraq haina usalama, hivyo inabidi wanajeshi vamizi wa Marekani wabakie nchini humo.

Ulinzi umeimarishwa Iraq baada ya magaidi wa ISIS kufanya mashambulizi mapya

 

Ikumbukwe kuwa, tarehe 5 Januari 2020, siku mbili baada ya wanajeshi magaidi wa Marekani kuwaua kidhulma makamanda wa muqawama wakiongozwa wa Luteni Jenerali Qassem Soleimani, Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mainduzi ya Kiislamu SEPAH, bunge la Iraq lilipasisha muswada wa kufukuzwa wanajeshi magaidi wa Marekani nchini humo. Pamoja na hayo zaidi ya mwaka mmoja umepita tangu kupasishwa muswada huo na bado mivutano ya kisiasa inaendelea kukwamisha utekelezaji wake. 

Baadhi ya makundi ya kisiasa na makundi ya muqawama ya Iran yanatilia mkazo wajibu wa kufukuzwa haraka wanajeshi vamizi wa Marekani nchini humo. Pamoja na hayo kuna baadhi ya makundi na wanasiasa ambao hata baadhi yao wamo serikalini, wanataka wanajeshi wa Marekani waendelee kubakia nchini humo. Inaonekana wazi kwamba, vitendo hivi vya kigaidi vinavyofanywa sasa hivi na magaidi wa Daesh huko Iraq, ni sehemu ya njama za kuhalalisha kubakia wanajeshi magaidi wa Marekani nchini Iraq na kusahaulisha uamuzi wa Bunge wa kutimuliwa wanajeshi hao vamizi. 

Fuad Hussein, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iraq amesema, tutaitaka serikali mpya ya Marekani iendelee na vikao vya mazungumzo ya kiistratijia na iteue timu mpya ya mazungumzo kuhusu wanajeshi wa Marekani waliopo Iraq.

Sehemu nyingine ya ulinzi mkali katika meidan ya al Tayran, Baghdad Iraq palipotokea mashambulio ya kigaidi

 

Suala jingine ni kwamba kuna ushahidi mwingi unaothibitisha kuwa Marekani imemimina nchini Iraq maelfu ya magaidi wa Daeshi kutokea Syria ili kuzuia kufukuzwa wanajeshi wa nchi hiyo huko Iraq. Sabah al Akili, mtaalamu wa masuala ya kiusalama ya Iraq anasema: Taarifa zilizothibitishwa zinaonesha kuwa, misafara ya kijeshi ya Marekani imemimina magaidi elfu 4 wa Daesh ndani ya Iraq kutokea Syria na askari wa Iraq hawakuruhusiwa kabisa kupekua malori ya misafara hiyo. Inavyoonesha ni kuwa, magaidi wa ISIS walioingizwa na Marekani nchini Iraq kutokea Syria ndio waliofanya mashambulizi ya kigaidi ya hivi karibuni na hiyo ndiyo sababu ya kuongezeka mashambulio hayo ya kigaidi huko Iraq hivi sasa.

Nukta nyingine ni kwamba, baada ya miripuko ya siku ya Alkhamisi ya mjini Baghdad, serikali ya Iraq na vikosi vya ulinzi vya nchi hiyo, vimejikita zaidi katika kulinda usalama wa mji mkuu huo. Upenyo huo umetumiwa vibaya na mabaki ya magaidi wa Daesh kufanya mashambulizi katika maeneo mengine ya nchi hiyo kama hilo lililovanyika kwenye kituo cha harakati ya al Hashd al Sha'abi huko Salahuddin, kaskazini mwa Iraq.

Brigedia Jenerali Yahya Rasoul, msemaji wa Komandi Kuu ya Majeshi ya Iraq

 

Sababu nyingine ni kwamba, ingawa magaidi wa ISIS wamesambaratishwa huko Iraq, lakini harakati za siku chache zilizopita zinaonesha kuwa, bado mabaki ya genge hilo yamejificha ndani ya jamii ya Iraq. Ijapokuwa ni vigumu kuliunda tena genge hilo na kulifanya kuwa na nguvu kama mwaka 2014, lakini magaidi waliobakia na uungaji mkono wa madola ajinabi pamoja na kuendelea ukosevu wa utulivu wa kisiasa ndani ya Iraq, ni mambo ambayo yanatumiwa na magaidi hao kufanya uhalifu nchini humo.

Amma nukta ya mwisho ni kwamba mapigano yaliyotokea Jumamosi usiku baina ya wanamapambano wa al Hashd al Sha'abi na magaidi wa Daesh huko Salahuddin Iraq, kwa mara nyingine yamethibitisha kwamba harakati ya wananchi ya al Hashd al Sha'abi iko chini ya mashinikizo makubwa ya madola ya kibeberu hususan Marekani, lakini pamoja na hayo iko imara katika kulinda ardhi usalama wa wananchi na wa ardhi yote ya Iraq.

Tags