Jan 28, 2021 07:25 UTC
  • Rais wa Uturuki: Jamii ya kimataifa ikomeshe uenezwaji chuki dhidi ya Uislamu

Rais Recep Tayyip Erdoğan wa Uturuki amekosoa vyombo vya kijamii vya Magharibi kugeuzwa kuwa jukwaa la kuenezea chuki dhidi ya Uislamu na chuki dhidi ya wageni na akaitaka jamii ya kimataifa ichukue hatua kuzuia mwenendo huo.

Erdoğan ameashiria kuenea mambo yaliyo dhidi ya Uislamu na ya ubaguzi wa rangi katika vyombo vya habari vya kijamii vya Magharibi na akasema: "jamii ya kimataifa inapasa ichukue hatua ili maafa kama ya Bosnia, Rwanda na Cambodia yasirudiwe tena."

Rais wa Uturuki ameeleza kuwa, sambamba na kuenea janga la dunia nzima la Covid-19, "kirusi cha ubaguzi wa rangi" nacho pia kinasambaa kwa kasi duniani; na akaongezea kwa kusema: jamii ya wanadamu inapita katika kipindi kigumu.

Erdoğan amesema, anatiwa wasiwasi na kuongezeka kwa hujuma dhidi ya misikiti na makanisa na akaeleza kwamba "ugaidi wa ubaguzi wa rangi" ni tishio la usalama kwa amani ya jamii.

Chuki dhidi ya Uislamu katika nchi za Ulaya

Amebainisha pia: "Uhalifu unaofanywa kwa taasubi na chuki dhidi ya baadhi ya matabaka ya jamii kwa sababu ya utambulisho wao wa kikabila, wa kidini, dhahiri za watu na tofauti ya lugha unaongezeka kila siku."

Kabla ya hapo, rais wa Uturuki aliwahi kugusia suala la uenezwaji chuki dhidi ya Uislamu katika nchi za Ulaya na akasema: "chuki dhidi ya Uislamu si tu zinatishia maisha ya mamilioni ya Waislamu barani Ulaya, lakini zimegeuka kuwa tobo jeusi ndani ya thamani na tunu za nchi za bara hilo".../

Tags