Jan 30, 2021 02:44 UTC
  • Ukosoaji wa kuchelewa wa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu kuhusu kadhia ya Palestina

Akizungumza Jumanne katika kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kilichoandaliwa kwa ajili ya kujadili masuala ya eneo la Asia Magharibi (Mashariki ya Kati) Ahmad Abu al-Ghait, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu au kwa jina jingine Arab League, alisema kuwa Wapalestina wamepitia mashinikizo makubwa yasiyo na mfano wake katika miaka minne ya utawala wa rais wa zamani wa Marekani, Donald Trump.

Mgogoro wa Palestina na utawala haramu wa Israel ndio mgogoro uliochukua muda mrefu zaidi katika ulimwengu wa leo. Chanzo cha mgogoro huo ni hatua ya Israel ya kuendelea kuteka na kukalia kwa mabavu ardhi za Wapalestina, ardhi ambazo zimeendelea kuwa finyu kila uchao kutokana na njama za utawala huo za kupora na kujenga katika ardhi hizo vitongoji vya walowezi wa Kizayuni.

Katika hali ambayo nchi za Kiarabu tokea muongo wa 1950 hadi muongo wa 1970 zilipigana vita visivyopungua vinne na utawala ghasibu wa Israel kwa ajili ya kuwatetea Wapalestina, lakini kadiri miaka ilivyozidi kupita na kuingia madarakani watawala vibaraka wa Kiarabu wasiojali matukufu ya Wapalestina, ndivyo taratibu suala la Palestina lilivyozidi kupoteza umuhimu mbele ya watala hao kwa kadiri kwamba hii leo hawalipi kabisa umuhimu wowote suala hilo.

Katika miaka ya karibuni, watawala hao wasaliti wameamua kujitoa mafichoni na kuweka hadharani siasa zao za kuboresha uhusiano na utawala ghasibu wa Israel ambao unaendelea kutekeleza jinai za kutisha dhidi ya Wapalestina wasiokuwa na mtu wa kuwatetea.

Ubalozi wa Marekani ukifunguliwa katika mji mtakatifu wa Quds

Kuhusu suala hilo, Ubalozi wa utawala haramu wa Israel ulifunguliwa mjini Abu Dhabi siku ya Jumapili nao utawala wa Imarati ukatangaza hadhari kwamba hivi karibuni utafungua ubalozi wake mjini Tel Aviv. Ama kwa kweli uamuzi wa nchi vibaraka za Kiarabu wa kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa Israel ni hiana na usaliti mkubwa uliofanywa na nchi hizo dhidi ya taifa la Palestina. Utawala wa Rais Donald Trump wa Marekani ulitoa pigo kubwa zaidi kwa Wapalestina katika kipindi cha miaka minne ya utawala wake. Kwa kupuuza azimio nambari 2334 la Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa, utawala huo ulitambua rasmi ujenzi haramu wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi za Wapalestina na wakati huo huo kukanyaga hadharani mpango wa kubuniwa mataifa mawili ya Israel na Palestina, ambao wenyewe umekuwa ukiutetea kwa miaka hii yote.

Mpango wa 'Muamala wa Karne' ambao kivitendo unapunguza pakubwa jiografia na ukubwa wa ardhi za Wapalestina na wakati huo huo kulenga moja kwa moja utambulisho wa kihistoria na kidini wa Palestina, ni moja ya huduma kubwa zilizotolewa na serikali ya Trump kwa utawala ghasibu wa Israel. Kwa mujibu wa mpango huo, Marekani inauchukulia mji mtakatifu wa Quds kuwa mji mkuu wa Israel, ambapo hata ilichukua uamuzi wa kuuhamishia ubalozi katika mji huo kutoka Tel Aviv. Ni wazi kuwa hatua ya nchi za Kiarabu ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa Israel katika mazingira hayo ni msaada na huduma kubwa kwa utawala huo kwa madhara ya taila la Palestina.

Ahmad Abu al-Ghait amesisitiza katika kikao cha Baraza la Usalama kwamba suala la Palestina limepuuzwa pakubwa na jamii ya kimataifa na kuwa kuna dhulma kubwa ambayo imefanyika katika uwanja huo. Kwa maana kwamba mgogoro wa Palestina unatazamwa kwa jicho la Israel pekee ni kana kwamba Wapalestina ambao ardhi zao zimeporwa na kukaliwa kwa mabavu na utawala huo hawapo kabisa, au kwa uchache wamelazimishwa kukubali ukandamizaji wanaofanyiwa na utawala huo ghasibu.

Imarati na Bharain zikitia saini mkataba wa usaliti wa kuanzisha uhusiano wa kawaida na Israel

Kwa kutilia maanani hali hiyo, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu amesema: 'Sisi tunaitaka serikali mpya ya Marekani irekebishe siasa zake mbovu kuhusu suala la Palestina na kulipa taifa la Palestina matumaini kwamba jamii ya kimataifa ingali inazingatia mapambano yao ya muda mfrefu kwa ajili ya kujipatia uhuru na utawala wa haki.'

Licha ya kuwa bado haijajulikana ni siasa zipi zitakazotekelezwa na serikali mpya ya Marekani kuhusu suala la Palestina, lakini siku moja tu baada ya kuidhinishwa kwake na Seneti ya Marekani kuwa waziri wa mambo ya nje wa nchi hiyo, Anthony Blinken alizungumza kwa njia ya simu na Gabi Ashkenazi waziri mwenzake Israel, na kumuhakikishia kwamba Marekani itaendelea kusimama na kuutetea utawala huo haramu kwa nguvu zake zote.

Nukta ya mwisho ni kwamba, hata kama ni vizuri kutumia jukwa la kimataifa kuwatetea Wapalestina wanaodhulumiwa, lakini ni wazi kuwa Palestina inahitajia uungaji mkono wa nchi na taasisi za Kiarabu kabla ya kuungwa mkono na Marekani, suala ambalo halijaonekana kabisa kutoka kwa nchi hizo katika miaka ya karibuni, bali zimekuwa zikitekeleza siasa ambazo zinaidhuru Palestina moja kwa moja. Hata Jumuiya ya Nchi za Kiarabu ambayo Abu al-Ghait ni katibu mkuu wake, imeshindwa kukosoa hatua iliyochukuliwa na Imarati na Bahrain tarehe 15 Septemba mwaka uliopita, kwa lengo la kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel.

Tags