Feb 10, 2021 23:35 UTC
  • UN: Uamuzi wa ICC umefungua mlango wa kupata haki Wapalestina

Ripota Maalumu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia masuala ya haki za binadamu katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu amesema uamuzi wa hivi karibuni wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC wa kubariki kuchunguzwa jinai za utawala wa kigaidi wa Israel dhidi ya taifa la Palestina umefungua mlango wa kupata haki Wapalestina.

Michael Lynk amesema hatimaye baada ya ngoja ngoja ndefu, ICC imetoa hukumu ambayo itafungua mlango wa kufanyika uchunguzi na hata kuwashitaki watendajii wa jinai hizo zinazokanyaga Mkataba wa Roma uliounda ICC.

Mtaalamu huyo wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya haki za binadamu huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu ameitaka jamii ya kimataifa iuunge mkono  uamuzi huo wa ICC ambao umefungua ukurasa wa kuanza mchakato wa kubebeshwa dhima wahusika wa jinai dhidi ya Wapalestina.

Mahakama ya ICC

Ijumaa iliyopita, majaji wa mahakama hiyo iliyoko mjini Hague nchini Uholanzi walitoa uamuzi wakisema kuwa mahakama hiyo ina mamlaka ya kisheria kuchunguza jinai za kivita katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na utawala huo ghasibu tokea mwaka 1967.

Uamuzi huo wa ICC ambao ni ushindi mkubwa kwa taifa la Palestina, umeukasirisha sana utawala wa kibaguzi wa Israel ambapo Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala huo ameishutumu korti hiyo yenye itibari ya kimataifa akidai kuwa hukumu hiyo imethibitisha kwa mara nyingine kwamba hiyo ni taasisi ya kisiasa na wala si ya kisheria.

Tags