Feb 16, 2021 02:41 UTC
  • Iraq yaitahadharisha Uturuki kuhusu mashambulizi dhidi ya Sinjar

Msemaji wa kikosi cha oparesheni za pamoja cha Iraq ameitahadharisha Uturuki kuhusu oparesheni ya jeshi katika eneo la Sinjar mkoani Nainawa huko Iraq na kueleza kuwa, Baghdad itachukua hatua zote za lazima iwapo itakabiliwa na shambulizi au uvamizi wowote wa nchi ajinabi.

Meja Jenerali Tahsin al Khafaji msemaji wa kikosi cha oparesheni za pamoja cha Iraq jana Jumatatu alisema kuwa, vikosi vyote vya ulinzi vimetumwa katika eneo la Sinjar na kwamba hali ya mambo imedhibitiwa na hakuna harakati yoyote ya hujuma ya silaha katika eneo hilo. 

Vikosi vya usalama vya Iraq vyawasili Sinjar  

Al Khafaji amesisitiza kuwa, hawataruhusu uvamizi na shambulio lolote katika ardhi ya Iraq na kwamba Baghdad itachukua hatua zote za lazima iwapo ardhi ya Iraq itashambuliwa. 

Al Khafaji amesema kuwa, vikosi vya usalama vya serikali kuu ya Iraq na vya eneo la Kurdistan nchini humo vinashirikiana kwa ajili ya kukabiliana na mashambulizi yoyote ya nchi ajinabi na yale ya ndani na kwamba hakuna mapatano yoyote ya siri kati ya Iraq na Uturuki. Amesema vikosi hivyo vinafanya juhudi ili kuilinda Iraq.  

Jeshi la Uturuki Jumatano iliyopita lilianza kutekeleza oparesheni yake mpya kwa jina la "Eagle Claw 2" katika eneo la Gara kaskazini mwa Kurdistan huko Iraq. Lengo la oparesheni hiyo limetajwa kuwa ni kukabiliana na mamluki wa chama Wakurdi wa Uturuki cha PKK. 

Tags