Feb 24, 2021 12:00 UTC
  • Rushwa ya chanjo ya Corona ya kwa mataifa ili yahamishie balozi Baytul-Muqaddas

Imefichuliwa kuwa, Waziri Mkuu wa utawala haramu wa Israel amekuwa akitoa kwa masharti chanjo ya Corona kwa mataifa ya dunia akiyataka yahamishie balozi zao kutoka Tel Aviv na kuzipeleka Baytul-Muqaddas.

Benny Gantz, Waziri wa Vita wa utawala haramu wa Israel amefichua kuwa, Waziri Mkuu huyo amekuwa akiitumia chanjo ya Corona kwa malengo yake ya kisiasa.

Gantz amesema kuwa Netanyahu amekuwa akitoa rushwa ya chanjo ya Covid-19 na kuyataka baadhi ya mataifa yahamishie balozi zao huko Baytul-Muqaddas na hivyo kujipigia debe kisiasa, hasa katika kipindi hiki ambapo umebakia muda wa chini ya mwezi mmoja kabla ya kufanyika uchaguzi wa Bunge.

Gantz ambaye ni hasimu wa kisiasa wa Benjamin Netanyahu ameitaja hatua hiyo kuwa ni biashara ya uchaguzi ambayo haikubaliki kwani ni kutumia fedha na kodi za wananchi kwa ajili ya malengo ya kisiasa.

 

Disemba mwaka 2017, aliyekuwa Rais  wa Marekani Donald Trump alichukua uamuzi wa upande mmoja wa kuutambua mji mtakatifu wa Quds kuwa mji mkuu wa utawala haramu wa Israel, na kutangaza kuhamishia ubalozi wa Washington  mjini Beitul-Muqaddas.

Licha ya propaganda kubwa ya mpango huo, hadi sasa ni nchi mbili tu za Guatemala na Paraguay ndizo ambazo zimefuata mkumbo huo wa Marekani huku Paraguay ikibadilisha uamuzi na kuurejesha tena ubalozi wake huko Tel Aviv ikiwa imepita miezi michache tu baada ya kuupeleka huko Baytul-Muqaddas.