Feb 25, 2021 03:38 UTC
  • Oparesheni ya Maʼrib, mapambano muhimu katika vita vya Yemen

Maʼrib ni eneo ambalo liko kaskazini mashariki mwa mji mkuu wa Yemen Sanaʽa na hivi sasa ni kitovu na medani kubwa ya mapigano biana ya wanajeshi wa muungano vamizi unaoongozwa na Saudia na Serikali ya Uwokozi wa Kitaifa ya Yemen

Vita vya muungano wa Saudia dhidi ya Yemen vilianza Machi 26 mwaka 2015 na mwezi ujao vita hivyo vitaingia katika mwaka wa saba. Hivi sasa medani kuu ya vita hivyo ni mkoa wa Ma'rib.

Saudi Arabia iliivamia Yemen kutokana na mahesabu ya kimakosa na kujitakia makuu mrithi kijana wa ufalme huo, ambaye alidhani kuwa angepata ushindi katika vita vya Yemen katika kipindi cha mwaka mmoja. Hivi sasa Saudia imefedheka kisiasa na kijeshi baada ya kutumbikia katika kinamasi cha vita ilivyoanzisha dhidi ya nchi masikini zaidi ya Kiarabu katika eneo la Asia Magharibi. Hivi sasa Saudia inafanya juu chini kuzuia ushindi wa Jeshi la Yemen na Kamati za Kujitolea za Wananchi huko Ma'rib.

Mpiganaji wa Ansarullah

Vita vya Ma'rib vina umuhimu mkubwa sana. Kanali Shamsan, mtaalamu wa masuala ya kijeshi wa Yemen anabainisha umuhimu wa vita vya Ma'rib kwa kusema: "Vita vya kukomboa Ma'rib vina umuhimu mkubwa na ni vyenye kuanisha hatima. Umuhimu huo hauhusiani tu na hujuma ya miaka kadhaa dhidi ya Yemen bali pia unahusu historia ya sasa ya Yemen. Hii ni kwa sababu mkoa huu umekuwa chini ya satwa ya Saudia kwa miongo kadhaa sasa."

Mbinu ya Saudia ya kujaribu kuzuia kushindwa na kupata pigo la kistraijia huko Ma'rib imekuwa ni kudondosha mabomu kila siku katika eneo hilo na kuomba msaada kutoka kwa magaidi kama  vile ISIS au Daesh ambao wamehamishwa kutoka mikoa mingine ya Yemen hadi Ma'rib.

Gazeti la Al Akhbar limeandika hivi kuhusu kadhia hii: "Ili kuzuia kukombolewa Ma'rib, Saudia imewaajiri maelfu ya magaidi kutoka mikoa mingine ya Yemen kama vile Shabwah, Abyan,  Hadhramaut, Aden, Lahij, Taiz na Pwani ya Magharibi." Gazeti hilo limeongeza kuwa Saudia inafanya juu chini kuhakikisha kuwa ngome yake ya mwisho kaskazini mwa Yemen inalindwa.

Katika kukabiliana na hali hiyo, Serikali ya Uwokozi wa Kitaifa ya Yemen imechukua hatua ambazo awali zimeiwezesha kupata ushindi katika vita vya kisaikolojia na hivyo hivi sasa iko katika hali ya juu ya kimotisha na kujiamini na inaelekea kukomboa Ma'rib kikamilifi na kusitisha ukaliaji mabavu wa Saudia katika mkoa huo.

Mohammad Abdul Salam, msemaji wa Harakati ya Ansarullah ya Yemen ambaye pia ni kiongozi wa ujumbe wa mazungumzo katika Serikali ya Wokozi wa Kitaifa ya Yemen ameandika hivi katika ujumbe wake wa Twitter: "Kutimuliwa wavamizi ajinabi ni jukumu la kila Myemen mpenda uhuru. Kwa ushirikiano wa wananchi, mikoa yote itakombolewa na adui hatakuwa tena na nafasi ili wote, kama walivyo wakaazi wa Ma'riba, waweze kuishi kwa heshima. Mikoa hii imekuwa ikitumiwa na wanajeshi wa adui kuwashambulia watu wa Yemen.

Ansarullah imechukua hatua muhimu kuhakikisha kwamba inapata ushindi katika vita vya Ma'rib na viongozi wengi wa kikabila katika eneo hilo wameafikiana na hatua hizo. Uungaji mkono wa makabila ya Ma'rib kwa oparesheni za Jeshi la Yemen kwa kushirikiana na  Kamati za Wananchi wa Yemen umepelekea jeshi hilo liweze kupata mafanikio katika matukio ya sasa huko Ma'rib.

Ndege ya kivita ya Saudia ikielekea Yemen

Maudhui nyingine ni kuwa, oparesheni ya Ma'rib imeweka wazi hitilafu kubwa zilizopo katika muugano vamizi unaoongozwa na Saudia. Iwapo Serikali ya Uwokozi wa Kitaifa ya Yemen itapata ushindi katika mkoa wa Ma'rib basi serikali hiyo itakuwa  imedhibiti mikoa 13 ya kaskazini mwa Yemen.

Kuhusiana na hili, gazeti la Al Akhbar limeandika: "Baraza la Mpito la Kusini mwa Yemen linalofungamana na Umoja wa Falme za Kiarabu halijatuma askari wake Ma'rib." Nukta hiyo inaashiria mgongano uliopo baina ya Saudia na Umoja wa Falme za Kiarabu katika vita vya Ma'rib.

Ushindi wa Jeshi la Yemen kwa kushirikiana na  Kamati za Wananchi wa Yemen katika oparesheni ya Ma'rib utaandaa mazingira ya jeshi hilo kudhibiti eneo la kijiografia la kaskazini mwa Yemen na hilo linaweza kupelekea kuanza mapigano mapya kusini mwa Yemen na hatimaye kuiwezesha Serikali ya Uwokozi wa Kitaifa kudhibiti nchi zima.