Feb 27, 2021 09:07 UTC
  • Shambulizi la anga la Marekani huko Syria, nembo ya kupenda vita ya serikali ya Biden

Mwaka 2014 Marekani ilituma majeshi yake kinyume cha sheria nchini Syria kwa kisingizio cha kupambana na kundi la kigaidi la Daesh na majeshi hayo yamebakia nchini humo hadi sasa licha ya wito wa mara kwa mara wa serikali ya Damascus wa kutaka kuondoka majeshi hayo vamizi katika ardhi yake.

Wakati huo huo Washington imekuwa ikishambulia vikosi vya muqawama vinavyopambana na magaidi nchini Syria, na licha ya nara zinazotolewa na rais mpya wa Marekani, Joe Biden, lakini kiongozi huyo pia ameamua kuchukua sera za kihasama na kiadui dhidi ya kambi ya muqawama na mapambano.

Alkhamisi iliyopita Wizara ya Ulinzi ya Marekani (Pentagon) ilitangaza kuwa, jeshi la nchi hiyo limeshambulia ngome za makundi ya muqawama huko Mashariki mwa Syria kwa amri ya Rais "Biden". Taarifa hiyo ilisema kuwa: "Kwa amri ya Rais Joe Biden, alasiri ya Akhamisi jeshi la Marekani limefanya mashambulizi ya anga dhidi ya taasisi zinazotumiwa na makundi yanayoungwa mkono na Iran huko Mashariki mwa Syria."  

Taarifa hiyo imeongeza kuwa: "Rais Biden atachukua hatua kulinda maafisa wa Marekani na waitifaki wake. Hatua yetu ni jibu la kimantiki lenye lengo la kupunguza mizozo huko Mashariki mwa Syria na Iraq."

Joe Biden

Ni dhahiri kwamba, hatua hiyo imechukuliwa kwa amri ya moja kwa moja ya Joe Biden kwa malengo kadhaa:

Kwanza ni kwamba Washington inadhani kuwa, shambulizi hilo la kijeshi ni jibu kwa mashambulizi ya karibuni yaliyolenga kambi na vituo vya Marekani nchini Iraq likiwemo lile lililolenga uwanja wa ndege wa Erbil. Baada ya shambulizi hilo Marekani ilidai kuwa makundi yenye mfungamano na Iran ndiyo yaliyohusika na kitendo hicho na ikasema itatoa jibu kali. Hii ni licha ya kwamba, Iran ililaani waziwazi shambulio hilo lililolenga uwanja wa ndege wa Erbil na kulitaja kuwa ni hatua ya kutiliwa shaka iliyokusudiwa kufanywa kisingizio cha kutetea uwepo wa majeshi ya Marekani nchini Iraq.

Ukweli ni kwamba, kwa sasa Marekani inawasaidia mabaki ya kundi la kigaidi la Daesh huko Iraq na Syria. Mtaalamu maarufu wa masuala ya usalama wa Iraq, Muayyad al Ali anasema: Jeshi la Marekani linawasaidia mabaki ya kundi la Daesh nchini Iraq kwa kuwapa taarifa na ripoti za kipelelezi zinazokusanywa na ndege zisizo na rubani za nchi hiyo.

Hata hivyo ni wazi kuwa, upinzani wa kuwepo majeshi ya Marekani nchini Iraq unaendelea kupamba moto hususan baada ya mauaji ya kigaidi yaliyofanywa na Marekani dhidi ya Luteni Jenerali Qassem Soleimani na Abu Mahdi al Muhandis Januari mwaka jana wa 2020. Baada ya mauaji hayo ya kigaidi yaliyokiuka sheria zote za kimataifa, Bunge la Iraq lilipasisha azimio la kufukuzwa majeshi ya Marekani katika ardhi ya nchi hiyo. Hata hivyo Washington imekataa kutekeleza kikamilifu azimio hilo na imebakisha wanajeshi 2,500 katika ardhi ya Iraq. 
Lengo la pili la mashambulizi ya juzi ya Marekani huko Syria ni kuuunga mkono utawala haramu wa Israel na matakwa yake ya kuondoka vikosi na makundi yote ya muqawama nchini Syria. Kwa muda sasa Israel imekuwa ikifanya mashambulizi ya anga ya mara kwa mara dhidi ya vituo vya makundi ya mapambano katika maeneo mbalimbali ya Syria. 

Sasa serikali ya Biden ambayo awali ilidai kutengua sera na siasa za serikali ya Donald Trump, inafuata nyayo za serikali ya mtangulizi wake ikiwemo sera za vita za Trump kuhusiana na Syria. Kuwepo kwa majeshi ya Marekani katika ardhi ya Syria ni kinyume cha sheria zote za kimataifa, hasa kwa kutilia maanani kwamba, Damascus inapinga vikali suala hilo na imewasilisha malalamiko yake katika taasisi za kimataifa. 

Magari ya jeshi la Marekani yakiiba mafuta nchini Syria

Majeshi ya Marekani yako maeneo ya Mashariki mwa Syria ambayo yana utajiri mkubwa wa mafuta na gesi na yamekuwa yakijishughulisha na uporaji wa utajiri huo. Mashambulizi ya karibuni ya Marekani huko Syria pia ni mashambulizi dhidi ya ardhi ya nchi inayojitawala na mwanachama wa Umoja wa Mataifa.

Kwa kuwa mashambuilizi haya yamefanyika bila ya idhini ya Umoja wa Mataifa, hapana shaka kuwa, yamekiuka sheria za kimataifa. Kwa amri hiyo ya kushambuliwa ardhi ya Syria, Biden ameonyesha kuwa, siasa za kupenda vita za Marekani hazibadiliki na ni sera thabiti ya serikali ya Washington bila ya kujali nani anayepangisha ikulu ya White house

Tags