Feb 27, 2021 12:03 UTC
  • Makundi ya muqawama Iraq yaapa kujibu chokochoko mpya za Marekani

Harakati za muqawama za Iraq zimelaani vikali mashambulizi ya anga ya jeshi la Marekani yaliyolenga kambi za makundi hayo ya kupambana na ugaidi katika mpaka wa Iraq na Syria, na kusisitiza kuwa, chokochoko hizo mpya za Washington hazitapita bila kupewa jibu kali.

Qais Khazali, kiongozi wa harakati ya Asa’ib Ahl al-Haq ya Iraq sanjari na kulaani hujuma hizo za anga za Marekani, ameeleza bayana kuwa, kitendo hicho kilichofanywa kwa maslahi ya utawala wa Kizayuni kwa mara nyingine kimeonesha kiwango cha sera za uhasama wa serikali mpya ya Washington dhidi ya Wairaqi.

Amesema njia pekee kwa taifa hilo la Kiarabu kupata uthabiti ni kuondoka vikosi vamizi vya Marekani nchini humo.

Wakati huohuo, harakati ya al-Nujabaa ya Iraq sambamba na kutoa mwito wa kuchunguzwa mashambulio hayo ya Marekani imeeleza bayana kuwa, jinai hiyo mpya ya Washington haitapita bila kupewa jibu.

Katika hatua nyingine, Wizara ya Ulinzi ya Iraq imeeleza kushangazwa kwake na madai ya Marekani kwamba hujuma hiyo ya jana ilifanyika kwa ushirikiano wa kiintelijensia wa Baghdad na Washington.

Wanajeshi vamizi wa Marekani nchini Iraq

Jeshi la Marekani kwa amri ya Rais Joe Biden usiku wa kuamkia jana Ijumaa lilifanya mashambulizi ya anga yaliyolenga makao makuu ya kundi la muqawama la Hashdu Shaabi linalopambana na magenge ya kigaidi katika mpaka wa Iraq na Syria.

Mbunge wa Iraq ambaye pia ni msemaji wa harakati ya Fat'h, Ahmed al-Asadi amesema uvamizi huo mpya wa Marekani dhidi ya Iraq umeua na kujeruhi watu 30.

Tags