Mar 02, 2021 12:26 UTC
  • Saudi Arabia: Chanjo ya corona ni sharti la kufanya ibada ya Hija mwaka huu

Waziri wa Afya wa Saudi Arabia ametangaza kuwa, kupata chanjo ya virusi vya corona ni sharti muhimu kwa watu wote wanaoazimia kutekeleza ibada ya Hija mwaka huu katika miji mitakatifu ya Makka na Madina.

Tangazo hilo limetolewa katika gazeti la Okaz, mwezi mmoja tu kabla ya kuwadia msimu wa ibada ya Hija. Hata hivyo Waziri wa Afya wa Saudia, Tawfiq bin Fawzan Al-Rabiah hakueleza idadi ya Waislamu watakaoruhusiwa kushiriki ibada ya Hija mwaka huu, na iwapo mahujaji hao watakuwa wa ndani ya Saudi Arabia pekee kama iliyokuwa mwaka jana au hata kutoka nje ya nchi hiyo.  

Ibada ya Hija ya mwaka jana haikushirikisha Waislamu kutoka maeneo mengine ya dunia kutokana na maambukizi ya virusi vya corona. Wakati huo serikali ya Saudi Arabia ilitangaza rasmi kwamba, wageni kutoka nchi za nje hawataruhusiwa kutekeleza ibada ya Hija kutokana na maambukizi ya virusi vya corona.

Mahujaji watakiwa kupata chanjo ya corona kabla ya kushiriki ibada ya Hija.

Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Hija na Umra ya Saudi Arabia ilisema: "Hija ya mwaka huu 2020 itashirikisha idadi ndogo ya mahujaji wa ndani ya nchi na wageni wachache wanaoishi nchini kutokana na kuendelea maambukizi ya ogonjwa wa COVID-19 ambao haujapatiwa chanjo wala dawa."

Karibu watu elfu kumi kutoka ndani ya Saudia pekee ndio walioshiriki katika ibada hiyo.

Waislamu zaidi ya milioni mbili na nusu walishiriki katika ibada ya Hija ya mwaka wa kabla yake.  

Mwezi Machi mwaka jana pia Saudi Arabia ilisimamisha ibada ya Umra kwa Waislamu kutokana na maambukizi ya virusi vya corona. 

Tags