Mar 03, 2021 08:01 UTC
  • Makundi ya Kipalestina yasisitiza kufanyika duru ya pili ya mazungumzo ya kitaifa huko Cairo

Makundi ya Kipalestina yamesisitiza juu ya udharura wa kufanyika duru ya pili ya mazungumzo ya kitaifa huko Cairo, Misri kama ilivyopangwa.

Fauz Barhum Msemaji wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) amesisitiza kuwa, makundi yote ya Palestina yamekubaliana kufanyika duru hiyo ya pili ya mazungumzo; na suala hilo liliashiriwa katika taarifa ya mwisho ya kikao cha karibuni huko Cairo na kwa msingi huo ni jambo la dharura kufanyika duru hiyo. 

Fauz Barhum, Msemaji wa Hamas 

Msemaji wa Hamas ameeleza kuwa, duru ya kwanza ya mazungumzo ilikuwa kwa ajili ya kuandaa mazingira ya kufanyika uchaguzi wa bunge, na ya pili ya mazungumzo iliyopangwa kufanyika mwezi huu wa Machi pia ni kwa ajili ya kuandaa uwanja wa kufanyika uchaguzi wa baraza la taifa. 

Fauz Barhum ameongeza kuwa, vikao na mazungumzo yote hayo yanafanyika kwa njia endelevu; na duru hii ya pili ya mazungumzo pia inapasa kufanyika katika muda uliopangwa. Hii ni kwa sababu, uchaguzi wa bunge pia ni msingi wa uchaguzi wa baraza la taifa.  Msemaji wa Hamas amesema, makundi ya Palestina hayataraji kuakhirisha tarehe ya kufanyika duru ya pili ya mazungumzo ya kitaifa huko Cairo mwezi huu wa Machi. 

Makundi 14 ya Palestina hivi karibuni yalifanya vikao kadhaa huko Cairo mji mkuu wa Misri na kusisitiza ulazima wa kufanyika uchaguzi kama msingi wa kuondoa migawanyiko ya kisiasa huko Palestina na kufikia mapatano ya kitaifa.   

Mahmoud Abbas Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina mwezi Januari alitangaza tarehe za kufanyika uchaguzi wa bunge, rais na baraza la taifa na kueleza kuwa, uchaguzi wa bunge utafanyika tarehe 22 mwezi Mei, wa rais Julai 31 na ule wa baraza la taifa pia tarehe 31 Agosti mwaka huu.

Tags