Mar 03, 2021 13:33 UTC
  • Gantz ahofia hatua ya mahakama ya ICC dhidi ya maafisa wa utawala wa Kizayuni wa Israel

Waziri wa vita wa utawala haramu wa Kizayuni wa Israel amesema ana wasiwasi juu ya hatua inayoweza kuchukiuliwa na Mahakama ya Kimataifa Jinai ICC dhidi ya maafisa wa utawala huo na akaongeza kuwa, upo uwezekano wa mahakama ya The Hague kuwafuatilia kisheria mamia ya maafisa wa Israel katika faili la jinai za kivita dhidi ya Palestina.

Benny Gantz ameyasema hayo leo katika mahojiano na shirika la habari la Reuters alipozungumzia uamuzi uliotangazwa mwezi uliopita na ICC wa kuthibitisha ustahiki wa mahakama hiyo ya jinai wa kuchunguza faili za jinai za kivita za Israel dhidi ya Wapalestina na kuutaja uamuzi huo kama "tukio hasi". Gantz amedai kwamba, Israel itafanya kila njia kuwalinda maafisa wake na mahakama hiyo.

Waziri wa vita wa Israel amekiri pia utawala wa Kizayuni unajaribu kuishinikiza ICC ijapokuwa si mwanachama wa mahakama hiyo ya kimataifa ya jinai na akatabiri kuwa, endapo uchunguzi huo utaanzishwa, mamia ya maafisa wa Israel walioko katika nchi zingine watakuwa hatarini kukamatwa.

Fatou Bensouda, Mkuu wa Mashtaka wa Mahakama ya ICC aliyekuwa akishughulia mpango wa kufuatilia kisheria jinai zilizofanywa na utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina, alijiuzulu wadhifa wake huo wiki mbili zilizopita kutokana na mashinikizo ya Tel Aviv.

Siku kadhaa zilizopita, tovuti ya Axius iliwanukuu maafisa wa Kizayuni na kuripoti kuwa, katika mazungumzo ya kwanza ya simu ambayo Benjamin Netanyahu alifanya na Rais Joe Biden wa Marekani, waziri mkuu huyo wa utawala wa Kizayuni aliitaka Washington iendeleze vikwazo vilivyowekwa na rais aliyetangulia wa nchi hiyo Donald Trump dhidi ya mahakama ya ICC.

Gazeti la Haaretz liliwahi kutoa orodha ya watu ambao kuna uwezekano wa kushtakiwa katika faili la uchunguzi wa jinai za kivita zilizofanywa na utawala haramu wa Israel dhidi ya Wapalestina katika Ufukwe wa Magharibi na Ukanda wa Gaza, ambapo katika orodha hiyo yanaonekana pia majina ya Benjamin Netanyahu, Benny Gantz, Moshe Ya'alon, Naftali Bennett na Avigdor Lieberman.../ 

Tags