Mar 04, 2021 04:13 UTC
  • Syria yatuma barua mbili kwa Baraza la Usalama katika kipindi cha masaa 72

Wizara ya Mambo ya Nje ya Syria imetuma barua mbili katika kipindi cha masaa 72 kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na Mwenyekiti wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kulalamikia hujuma dhidi ya mji wa Damascus.

Mapema Ijumaa, Wizara ya Ulinzi ya Marekani ilitangaza kuwa, kwa amri ya Rais Joe Biden, jeshi la nchi hiyo lilishambulia kwa mabomu ngome za makundi ya muqawama mashariki mwa Syria.

Kanali ya Telegram ya Sabirin News ambayo iko karibu na makundi ya muqawama na mapambano ya Kiislamu imetangaza kuwa, ndege za kivita za Marekani zilidondosha mabomu katika eneo ambalo liko baina ya Bukamal na Al Qaim katika mpaka wa Syria na Iraq ambapo mtu mmoja aliuawa shahaidi na wengine wanne walijeruhiwa. Hali kadhalika mapema Jumapili, ndege za kivita za utawala wa Kizayuni wa Israel zilidondosha mabomu  mashariki mwa Damascus baada ya kuingia Syria kupitia eneo linalokaliwa kwa mabavu la Milima ya Golan.

Punde baada ya hujuma ya Marekani Ijumaa, serikali ya Syria iliandika barua mbili, moja kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na ya pili kwa mwenyekiti wa Baraza la Usalama la umoja huo ambapo ilikosoa uvamizi huo. Aidha baada ya hujuma ya Jumapili ya utawala dhalimu wa Israel, Syria pia imeandika barua nyingine kwa Umoja wa Mataifa ikilalamikia uvamizi huo.

Mashambulizi hayo yaliyo kinyume cha sheria ya Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Syria yamefanyika katika hali ambayo makundi ya kigaidi Syria yamedhoofika. Kwa msingi huo mashambulizi hayo ya Marekani na Israel yanalenga kusaidia makundi ya kigaidi na kuyapa motisha wa kupambana na Jeshi la Syria na waitifaki wake.

Ngao wa kujihami angani ya Syria ikitungua kombora la Israel mjini Damascus

Mashambulizi hayo ni ukiukwaji wa wazi wa mamlaka ya kujitawala ya Syria na pia ni hatua inayoashiria kutotambuliwa rasmi mamlaka ya serikali iliyoko madarakani Damascus chini ya Rais Bashar al Assad. Utawala wa Kizayuni wa Israel na baadhi ya tawala  za Kiarabu na za Magharibi katika muongo mmoja  uliopita zimekuwa zikifanya jitihada kubwa sana kuiangusha serikali halali ya Rais Assad lakini zimegonga mwamba. Kwa msingi huo katika miaka miwili iliyopita zimekuwa zikifanya kila ziwezalo kuidhoofisha serikali ya Damascus na kuizuia kuwa na satwa pamoja na mamlaka kamili katika maeneo yote ya kijiografia ya Syria. Ni kwa msingi huo ndio katika barua ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Syria kwa Umoja wa Mataifa, moja kati ya nukta zilizosisitizwa ni haki ya Syria ya kulinda ardhi na wananchi wake kwa mbinu zozote zinazowezekana kwa mujibu wa Hati ya Umoja wa Mataifa.

Nukta nyingine hapa ni kuwa, mashambulizi ya utawala haramu wa Israel na Marekani dhidi ya Syria yanajiri wakati ambao nchi hii sawa na aghalabu ya nchi nyingine nyingi duniani inakabiliana na janga la corona. Kwa hakika mashambulizi hayo yanaonyesha kuwa Marekani na Israel hazijali kuhusu maisha ya raia wa nchi nyingine duniani.

Kuhusiana na nukta hii, Bassam al-Sabbagh mwakilishi wa kudumu wa Syria katika Umoja wa Mataifa, akilihutubu Baraza la Usalama la umoja huo baada ya hujuma hiyo ya Ijumaa ya Marekani alikosoa vitendo vya wanajeshi vamizi dhidi ya nchi yake na kusema hali ya kibinadamu nchini Syria inapuuzwa kwa makusudi.

Rais Bashar al Assad wa Syria

Hujuma ya Israel nchini Syria imejiri punde baada ya hujuma ya Marekani na hivyo ni wazi kuwa kulikuwa na ushirikiano baina ya Washington na Tel Aviv katika uvamizi huo.

Katika upande mwingine, Israel imekuwa ikiihujumu Syria mara kwa mara lakini jamii ya kimataifa imenyamazia kimya ukiukwaji huo wa sheria za kimataifa.

Katika barua ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Syria kwa Umoja wa Mataifa kufuatia hujuma ya hivi karibuni ya Israel, nukta muhimu iliyotajwa ni kuwa hujuma hiyo dhidi ya mkoa wa Deir ez Zour imefanyika kwa uungaji mkono wa Marekani na baadhi ya nchi za Kiarabu. Aidha Syria imesema utawala wa Israel umepata ujasiri wa kutenda jinai hiyo kwa sababu unafahamu kuwa hautawajibishwa.

Mwisho tunaweza kusema kuwa, serikali mpya ya Marekani inaunga mkono hatua zilizo kinyume cha sheria za Israel dhidi ya nchi zingine hasa Syria.

Inaelekea kuwa  sera za utawala wa Joe Biden katika eneo la Asia Magharibi zitapelekea kuongezeka vita vya niaba katika eneo. Kwa msingi huo hatua za Israel dhidi ya Syria ni katika fremu ya kufikia lengo hilo hilo.

Tags