Mar 04, 2021 04:15 UTC
  • Palestina: Silaha za Israel zimetumika kuua Waislamu na wapinzani wa mapinduzi Myanmar

Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Palestina imeituhumu Israel kuwa inauuzia silaha utawala wa Myanmar ambazo zimetumika kuua Waislamu wa jamii ya Rohingya na vilevile kuua wapinzani wa mapinduzi ya kijeshi yaliyotokea nchini humo, licha ya marufuku ya kimataifa ya kuiuzia silaha nchi hiyo.

Taarifa ya Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Palestina imesema kuwa, utawala wa Israel haukuchukuliwa hatua kwa kukiuka marufuku ya silaha ambazo zimetumiwa kutoa roho za maelfu ya Waislamu wasio na hatia kama ambavyo zinatumika sasa kuwatia wahka na hofu raia wanaopinga mapinduzi ya kijeshi, kutoa roho zao na kujeruhi wengine wengi.

Taarifa ya Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Palestina imelitaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linalojitayarisha kuitisha kikao cha kujadili hali ya Myanmar, lisitosheke kutaja majina ya vinara wa mapinduzi huko Myanmar bali pia liashirie viongozi wa utawala ghasibu wa Israel waliotayarisha zana na silaha zilizotumiwa kufanya mapinduzi hayo na kukandamiza wananchi.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa, utawala ghasibu wa Israel unaoziuzia silaha tawala za kidikteta zinazotumiwa kukandamiza raia na kuwanyima uhuru wao, unazifanyia majaribio silaha hizo kwa kuwaua raia wa Palestina na kukandamiza maandamano yao ya amani.

Tags