Mar 04, 2021 06:08 UTC
  • Waziri wa Mambo ya Nje wa Yemen: Mgogoro wa sasa nchini ndio mbaya zaidi wa binadamu katika zama za sasa

Waziri wa Mambo ya Nje wa Serikali ya Uokovu wa Kitaifa ya Yemen amesem kuwa, hali ya sasa ya nchi hiyo inaashiria maafa mabaya zaidi ya binadamu ambayo hayajawahi kushuhudiwa katika zama za sasa.

Hisham Sharaf ambaye alikuwa akihutubia kikao cha nchi wafadhili amesema kuwa, kiwango cha misaada iliyotolewa hadi sasa kwa ajili ya Yemen ni kidogo sana na kinavunja matumaini.  

Sharaf amesema jamii ya kimataifa inaendelea kuwa mtazamaji tu mbele ya maafa ya watu wa Yemen huku nchi vamizi zinazoongozwa na Saudi Arabia zikiendelea kushambulia raia wasio na hatia. Amesema nchi za dunia zinaendelea kuzungumzia maafa ya kibinadamu ya Yemen bila ya kuwa na azma ya kushughulikia sababu za maafa hayo.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Yemen amesema sababu kuu ya maafa ya sasa ya Yemen ni mashambulizi ya anga na nchi kavu yanayofanywa kwa kutumia silaha zilizopiga marufuku na vilevile mzingiro wa pande zote wa Saudia na washirika wake dhidi ya taifa la Yemen.

Amesema kuwa mzingiro wa pande zote dhidi ya Yemen, kuzuia meli zinazobeba bidhaa muhimu kama mafuta ya petroli, kufungwa uwanja wa ndege wa San'aa na kupunguzwa thamani ya sarafu ya Yemen ni baadhi ya sababu za maafa ya sasa ya nchi hiyo. 

António Guterres Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa akizungumza Jumatatu katika ufunguzi wa kikao cha kimataifa cha kukusanya misaada ya kifedha kwa ajili ya Yemen, alitoa wito kwa wafadhili kujitolea zaidi ili nchi hiyo ya Kiarabu isitumbukie katika njaa na maafa makubwa.

Watoto wa Yemen...

Guterres mesema: "Leo kukatwa au kupunguzwa misaada ya kibinadamu kwa ajili ya Yemen ni sawa na kutoa hukumu ya kifo kwa wakaazi wa nchi hiyo." 

Kwa mujibu wa takwimu za hivi karibuni za Umoja wa Mataifa, zaidi ya Wayemen milioni 16 au takribani nusu ya watu wote milioni 29 wa nchi hiyo wanakabiliwa na baa kubwa la njaa.

Aidha takwimu za Umoja wa Mataifa zinaonyesha kuwa, watu nusu milioni nchini Yemen wanakaribia kufa kutokana na njaa huku watoto zaidi ya lakini nne walio na umri wa chini ya miaka mitano nao pia wakiwa katika hatari ya kupoteza maisha iwapo hali ya hivi sasa itaendelea.