Mar 04, 2021 13:15 UTC
  • Jeshi la Yemen lashambulia tena shirika la mafuta la Saudia ARAMCO

Msemaji wa vikosi vya ulinzi vya Yemen leo Alkhamisi ametangaza habari ya kufanyika shambulio jingine katika taasisi za mafuta za Saudi Arabia, ARAMCO.

Televisheni ya al Aalam imemnukuu Brigedia Jenerali Yahya Saree akitangaza habari hiyo na kuongeza kuwa, shambulizi hilo limefanyika kwa mafanikio katika eneo lililoainishwa kabla, la taasisi za mafuta za Saudia.

Amesisitiza kuwa, shambulizi hiyo ni majibu ya kawaida kabisa ya wananchi wa Yemen ambao kila leo wanafanyiwa jinai za kila namna na wavamizi wa nchi yao hasa Saudi Arabia.

Pia amesema, shambulio la leo Alkhamisi limelenga taasisi za mafuta za Aramco mjini Jeddah na kombora la Quds2 ndilo lililotumika kwenye shambulio hilo.

Athari za mashambulizi ya wanamapambano wa Yemen katika shirika la mafuta la Saudia ARAMCO

 

Huku hayo yakiripotiwa, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Serikali ya Wokovu wa Kitaifa ya Yemen amesema kuwa, sehemu kubwa ya mji wa kiistratijia wa Ma'rib imeshakombolewa na yamebakia maeneo machache tu.

Shirika la habari la FARS limetangaza habari hiyo leo na kumnukuu Hussein al Izzi akisema hayo na kufafanua kuwa, hadi hivi sasa, maeneo 10 kati ya 14 ya mji wa kiistratijia wa Ma'rib huko Yemen, yameshakombolewa.

Operesheni ya kuukomboa mkoa wa kiistratijia wa Ma'rib ambao una utajiri mkubwa wa mafuta, ni ushindi mkubwa na wa haraka linaopata jeshi na kamati za kujitolea za wananchi wa Yemen katika viunga vya mji wa Ma'rib umeitia kiwewe serikali ya watoro ya Mansour Hadi na mabwana zao.

Habari nyingine kutoka Yemen zinasema kuwa, kumetokea mripuko wa bomu katika mji wa Aden wa kusini wa nchi hiyo. Gari lililosheheni mabomu la mamluki wa Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) ndilo lililotumika kwenye shambulizi hilo.