Mar 06, 2021 02:54 UTC
  • Al-Wefaq: Mpango wa Bahrain wa kuunda muungano dhidi ya Iran ni usaliti

Harakati ya Kitaifa ya al-Wefaq ya nchini Bahrain imekosoa vikali mpango wa utawala wa Aal-Khalifa wa nchi hiyo wa kuungana na Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu na utawala haramu wa Israel kubuni eti muungano dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kusisitiza kuwa kitendo hicho ni usaliti.

Taarifa iliyotolewa jana na harakati hiyo imesisitiza kuwa, mpango huo wa kiujiunga na muungano wa kiuadui dhidi ya Iran unakwenda kinyume na thamani za kitaifa za Bahrain. 

Taarifa hiyo imeeleza bayana kuwa, harakati, makundi na vyama vyote vya Bahrain vinapinga njama hizo za kufanya urafiki na utawala wa Kizayuni.

Kadhalika chama hicho kikubwa zaidi cha Kiislamu cha Bahrain kimesema hakuna nafasi ya utawala wa Kizayuni wa Israel nchini humo na kusisitiza kuwa wananchi wa Bahrain wataendelea kuwaunga mkono wananchi madhulumu wa Palestina.

Bahrain na Imarati zilivyojidhalilisha kwa kuanzisha uhusiano na Israel huko US mwaka jana (2020)

 

Harakati hiyo ya Kiislamu imesisitiza kwamba, raia wa Bahrain wanapinga aina yoyote ya kufanya uhusiano na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Taarifa ya Harakati ya Kitaifa ya al-Wefaq ya nchini Bahrain imebainisha kuwa, jitihada zozote za kucheza na kufuata mdundo wa ngoma ya utawala huo ghasibu zinazonesha udhaifu na idhilali ya utawala wa Aal-Khalifa kwa namna inavyojikomba kwa Wazayuni.