Mar 06, 2021 02:55 UTC
  • Rais wa Iraq: Hatutaruhusu kuenea ugaidi na misimamo ya kufurutu ada kwa jina la dini

Rais Barham Salih wa Iraq amesisitiza kuwa, nchi yake itaendeleza vita na mapambano dhidi ya ugaidi na misimamo ya kufurutu ada.

Rais wa Iraq amesema hayo katika hafla ya kumlaki Papa Francis Kiongozi wa Kanisa Katolikki Duniani aliyewasili jana nchini Iraq katika safari yake ya kihistoria katika nchi hiyo ya Kiarabu.

Rais Salih amesema, Wairaq Wakristo wa mashariki mwa nchi hiyo wamekuwa wakilalazimika kuikimbia nchi yao kutokana na mazingira mabaya yanayotawala ya ukosefu wa amani katika maeneo hayo.

Sambamba na kuashiria matokeo mabaya ya kuendelea kuhajiri wananchi wa Iraq wa mashariki mwa nchi Rais Barham Salih amesisitizxa kuwa, serikali yake inajitahidi kwa kadiri ya uwezo wake kutoruhusu kuenea misimamo ya kufurutu ada nchini humo kwa kutumia vibaya jina la dini na kwamba, katu nchi hiyo haitakubali dhulma.

Papa Francis, Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani akiwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Baghdad

 

Kwa upande wake, Papa Francis, Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani amesema kuwa, janga la virusi vya Corona ambalo linaisumbua dunia kwa sasa linahitajia mshikamano ili kukabiliana nalo.

Aidha ameashiria ugaidi na vitendo vya kufurutu ada ambavyo kwa miaka kadhaa sasa vinaitesa Iraq na kusema kuwa, kuna haja ya kutumiwa kwa njia sahihi uwepo wa dini mbalimbali, kaumu na tamaduni tofauti kwa ajili ya kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazoikabili nchi hiyo.

Papa Francis jana aliwasili Baghdad mji mkuu wa Iraq kwa safari ya siku tatu. Safari hii inahesabiwa kuwa ni ya kihistoria hasa kwa kutilia maanani kwamba, ni mara ya kwanza katika historia kwa Papa kuitembelea Iraq.