Mar 06, 2021 02:55 UTC
  • HAMAS: Tuna uhusiano mzuri sana na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran

Osama Hamdan, mjumbe wa ngazi za juu wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) amesema kuwa, harakati hiyo ina uhusiano mzuri na imara na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Kiongozi huyo mwandamizi wa Hamas amesema hayo katika mahojiano yake na Kanali ya Televisheni ya al-Mayadeen na kubainisha kwamba, pande mbili hizo zimekuwa zikishirikiana katika muqawama na mapambano dhidi ya utawala haramu wa Israel.

Aidha amesema, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran si tu kwamba haitaki chochote katika uhusiano wake na wananchi wa Palestina bali imekuwa na unyeti maalumu kuhusiana na malengo matukufu ya Palestina.

Osama Hamdan amesema, hivi sasa eneo la Mashariki ya Kati lipo katika hatua ya kuingia katika mabadiliko muhimu na kwamba, serikali mpya ya Marekani  itaunda muungano mpya kwa uongozi wa Israel ili kusukuma mbele gurudumu la kuanzisha uhusiano wa kawaida na Israel.

Ismail Hania, Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya HAMAS akisalimiana na Ayatullah Sayyid  Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika moja ya safari zake hapa Iran

 

Hii si mara ya kwanza kwa kiongozi wa ngazi za juu wa Hamas kuelezea uhusiano mzuri uliopo baina ya harakati hiyo na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Mkuu wa Idara ya Kisiasa ya harakati ya Hamas, Ismail Hania pia amekuwa akisisitiza mara kwa mara kwamba, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran daima imekuwa ikiyasaidia na kuyaunga mkono makundi ya wanamapambano wa Palestina na kwamba, Iran imetoa mchango mkubwa katika kuimarisha harakati ya Hamas. 

Tags