Mar 06, 2021 11:00 UTC
  • Safari ya Papa Francis nchini Iraq, wito wa kuishi pamoja kwa amani wafuasi wa dini tofauti

Katika miaka ya karibuni nchi ya Iraq imekuwa uwanja wa mashambulio na harakkati ya makundi ya kigaidi na kitakfiri hususan kundi la Daesh ambalo limesababisha madhara makubwa kwa nafsi na mali za wananchi wote wa nchi hiyo, Waislamu na Wakristo.

Safari ya Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francis, huko Iraq mbali na kusisitiza umuhimu wa kulaaniwa ugaidi na kuonyesha mshikamano na wahanga wa ugaidi, vilevile inatayarisha uwanja mzuri wa kuimarishwa hali ya kuishi kwa amani makundi ya wafuasi wa dini tofauti. 

Papa Francis aliwasili Baghdad Ijumaa ya jana tarehe 5 Machi na kulakiwa na Waziri Mkuu wa Iraq, Mustafa al Kadhimi. Katika safari hiyo ya siku tatu kiongozi wa Kanisa Katoliki atakutana na Wakristo wa Iraq, viongozi wa kidini na maafisa wa serikali ya nchi hiyo. Kabla ya safari hiyo Papa Francis alisema anataka kukutana na watu waliokumbana na mashaka mengi katika miaka ya hivi karibuni. 

Malengo ya safari ya Papa Francis nchini Iraq yanaweza kufupishwa katika nukta kadhaa. Kwanza ni kuwa Wakristo wa Iraq ni miongoni mwa wahanga wa ukatili wa makundi ya kigaidi katika miaka ya karibuni nchini Iraq na hapana shaka kuwa, kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki duniani anataka kuonyesha mshikamano na Wakristo hao katika safari yake ya sasa nchini Iraq. Katika safari hii Papa Francis mbali na kutoa heshima kwa wahanga wa machafuko ya miaka ya karibuni nchini Iraq, amesema: "Ninakuja kati yenu kama msafiri wa amani, nakuja kukariri kaulimbiu ya 'ninyi nyote ni ndugu,". Vilevile ametangaza mshikamano wake na jamii ya Wayazidi ambao amesema, wamepatwa na masaibu mengi.

Wakati wa uvamizi wa majeshi ya Marekani dhidi ya Iraq mwaka 2003, Wakristo walikuwa wakiunda asilimia karibu 6 ya jamii ya watu milioni 25 wa nchi hiyo. Hata hivyo baada ya vita na machafuko ya miaka kadhaa nchini humo, jamii ya Wakristo wa Iraq imepungua na kufikia watu karibu laki nne. Makundi ya kigaidi hususan Daesh yalifanya mauaji na ukatili mkubwa dhidi ya Wakristo katika maeneo mbalimbali ya Iraq na kuharibu makanisa mengi ambayo baadhi yalikuwa na thamani kubwa katika mtazamo wa kihistoria.

Lengo la pili la safari ya Papa Francis nchini Iraq ni kupanua zaidi anga ya kuishi pamoja kwa amani baina ya wafuasi wa dini tofauti. Katika uwanja huo Papa ametembelea eneo la Nasiriyah huko kusini mwa Iraq kwa shabaha ya kuzuru eneo la Ur ambako ndiko alikozaliwa Nabii Ibrahim (as) na kukutana na baadhi ya viongozi wa kidini wa eneo hilo. Balozi wa Iraq huko Vatican, Rahman Farhan al A'miri anasema: Ujumbe mkubwa wa safari ya Papa nchini Iraq ni kutangaza uungaji mkono wake kwa mazungumzo baina ya dini tofauti. Hii ni kwa sababu kiongozi huyo wa Kanisa Katolikki anasisitiza suala la kuimarishwa mazungumzo na maelewano baina ya dini mbalimbali.

Pamoja na hayo, suala muhimu kuliko yote katika safari ya sasa ya Papa Francis nchini Iraq ni kukutana na pia mazungumzo yake na kiongozi mkuu wa Waislamu wa Iraq, Ayatullah Sayyid Ali Sistani.

Image Caption

Mazungumzo hayo ya faragha yamekutanisha vinara wawili wa ulimwengu wa Kikristo na Kiislamu tena katika mji mtakatifu wa Najaf. Mazungumzo hayo yana umuhimu mkubwa hasa kwa kutilia maanani kwamba Papa Francis na Ayatullah Ali Sustani wana mtazamo unaofanana wa kulaani na kupinga vikali ugaidi na mizimamo ya kufurutu mipaka. Shakhsia hao wawili daima wamekuwa wakitilia mkazo suala la wafuasi wa dini mbalimbali kuishi pamoja kwa amani. Suala hili linapata umuhimu zaidi hususan kwa kutilia maanani nafasi muhimu ya Ayatullah Ali Sistani katika kurejesha amani na usalama nchini Iraq na wito wake wa udharura wa kupambana na ugaidi wa kundi la Daesh, kulinda ardhi yote ya Iraq na kujikomboa kutoka kwenye udhibiti wa madola ya kibeberu.

Tags